Sharifa Marira, Dodoma
Maalim Seif Shariff Hamad |
WANACHAMA wa CUF
wasiomwunga mkono Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba
wametangaza kwenda kwa mbwembwe na kujidai katika ofisi za chama hicho,
Buguruni, Dar es Salaam Aprili 30 ‘kufanya usafi’.
Usafi huo unahusu
pia kusafisha watu wote ambao chama hakiwatambui akiwamo Profesa Lipumba ambaye
alijiuzulu nafasi yake, hivyo wanachama zaidi ya 7,000 wa nchi nzima watakuwa
katika ofisi hiyo kufanya usafi na kuanza kazi rasmi.
Hayo yalisemwa
jana kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa na wabunge wa CUF wanamwunga mkono
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, walipokuwa wanazungumza
na waandishi wa habari.
Mbunge wa
Temeke,Abdallah Mtolea alisema siku hiyo wanachama wa CUF walio wengi watafanya
usafi kwani tangu Lipumba alipotambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi wasiomtambua hawajaenda ofisini hapo jambo linalosababisha
ofisi hiyo kuvamiwa na genge la wahuni.
“Mnaona makundi
yanakwenda kufanya fujo na kupiga watu na mle ndani kuna uchafu mwingi,
hatutaki ofisi yetu iendelee kuharibiwa,’’ alisema Mtolea.
”Wazo hilo
lilianzishwa na wanachama wa Temeke nikalikubali, lakini wanachama wa maeneo
mengine baada ya kusikia wamelipokea na wanataka kushiriki, hivyo tutaondoa
uchafu wote,’’ aliongeza.
Alisema
wanachama hao watakwenda na mafagio, madekio na vifaa vingine vya usafi, hawapangi
kufanya uovu siku hiyo na hakuna tukio la uvunjifu wa amani linalokwenda
kufanyika.
Alisema kaulimbiu
ya siku hiyo ni ‘Lipumba hakubaliki’ na wabunge wa CUF 40 ambao hawamwungi
mkono kiongozi huyo, watahudhuria siku hiyo.
“Maana ya uchafu
ni kitu chochote ambacho hakiko sehemu inayotakiwa, kwa hiyo kama kuna mtu
hastahili naye yupo pale maana yake naye ni uchafu anatakiwa aondoke.
Alisema hakuna
tamko lililotolewa na mtu yeyote kuwa wanachama ambao hawamkubali Lipumba
wasifike ofisini nasi tunaokwenda ni wanachama halali, kama Lipumba anajitambua
na anajiona ni Mwenyekiti, apokee wanachama na si kuwakimbia.
Akizungumzia kama
tukio hilo halitaharibu kesi mahakamani ya kupinga uamuzi wa Jaji Mutungi wa
kumrudisha Lipumba katika nafasi hiyo, alisema wana imani na Mahakama
katika kutoa haki ya kesi hiyo na kwamba tukio hilo haliwezi kuharibu chochote
kwani wanakwenda ofisini kwao.
Mbunge wa
Malindi, Ally Saleh alisema: “Ile ofisi ni yetu tunarudi kwenye ofisi yetu, si
mahali pengine sasa wakati umefika kwenda ofisini na hivyo hatuwezi kuingia
ikiwa chafu,tunasafisha ili tupate sehemu ya kufanyia siasa.
“Uamuzi wetu CUF
umefika wakati lazima twende katika ofisi yetu kuu ya Buguruni, tunataka kwenda
mzofafa yaani kwenda kwa mbwembwe na kujidai,’’ aliongeza.
Akizungumzia
tukio la kuvamiwa kwa waandishi wa habari kwenye mkutano wa hivi karibuni, aliomba
wote ambao hawakufurahishwa na tukio hilo, walaani na kwamba serikali
haijaonesha kuchukizwa nalo.
0 comments:
Post a Comment