*Asema kumpora shamba ni njama na hila za kumdhoofisha
*Aapa kutorudi CCM
na badala yake atahakikisha inang’oka
Salum Maige, Geita
Frederick Sumaye |
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema uamuzi wa Serikali
kumnyang’anya mali zake likiwamo shamba la Mabwepande, Dar es Salaam ni njama
na hila za CCM kumdhoofisha kisiasa baada ya kuhamia Chadema.
Amesema Oktoba mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, chini ya Waziri William Lukuvi
ilimnyang’anya shamba kwa madai ya kulimiliki muda mrefu bila kuliendeleza.
Akizungumza juzi kwenye kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), mkoa wa Geita kujadili hali ya demokrasia nchini, Sumaye alisema hata wakimnyang’anya mali wasitarajie kuwa atafilisika na kamwe hatarudi CCM.
Akizungumza juzi kwenye kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), mkoa wa Geita kujadili hali ya demokrasia nchini, Sumaye alisema hata wakimnyang’anya mali wasitarajie kuwa atafilisika na kamwe hatarudi CCM.
Sumaye aliyekuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, alisema
licha ya kunyang’anywa shamba hilo, ataendelea kuishi na maisha yake
hayatabadilika na akaahidi kupambana usiku na mchana kuhakikisha CCM inaondoka
madarakani.
“Mimi walininyang’anya shamba langu, nikawaambia
nyang’anyeni, mimi ndiyo sasa naingia kwenye mapambano sawasawa,” alisema
Sumaye na kuongeza:
“Wako marafiki zangu kule CCM wakahoji kwa nini nisirudi
CCM badala ya kuteseka kiasi hicho. Na mimi jibu nililowaambia ni moja tu, nimetoka
CCM kazi yangu iliyobaki ni kuiondoa CCM madarakani na si kurudi CCM.”
Alifafanua kuwa mateso wanayopata wananchi ndiyo wanayopata
viongozi wa juu wa Chadema ambao baadhi yao wameanza kuteswa kwa kunyang’anywa
mali zao akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyenyang’anywa nyumba
anayoimiliki kwa asilimia 75.
Alisema licha ya Mbowe kunyang’anywa nyumba hiyo ambayo
hakuitaja, alisema Serikali ina mpango wa kumpora pia shamba analolima kilimo
cha kisasa.
Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Sumaye ambaye ni
mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema Taifa, alisema uamuzi wa Rais John Magufuli
kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano kwa wananchi, ni kinyume na Katiba
ya Tanzania na haijawahi kutokea hali hiyo tangu vyama vingi vilipoanzishwa.
Alisema kwa katazo hilo, hakuna mtu atakayeanzisha chama
cha siasa kwani kuanzisha chama lazima ifanyike mikutano ya hadhara kutafuta
wananchi, lakini kwa hali hiyo hakutakuwa na usajili wa vyama.
“Hata Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mtungi
anajua hilo kwamba demokrasia imekandamizwa. Nasi hatuogopi kumwambia Rais
ambayo si ya kufanya kwani hana ruhusa ya kuvunja Katiba kwani aliapa kuilinda
na kuitetea,” alisema Sumaye.
Aidha, alisema kama hali itaendelea hivyo pamoja na hali
ngumu ya maisha ya Watanzania njia itakuwa nyeupe ya Chadema kuingia
madarakani, na hivyo aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuipinga Serikali na
kutetea demokrasia.
Baadhi ya wananchi walisema hali ya maisha ni ngumu na
imefikia hatua ya wanaume kutelekeza familia zao kwa kushindwa kuzihudumia.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) jimbo la
Geita, Mary Paschal alisema kuna familia zimetelekezwa na wanaume kwa sababu ya
maisha magumu.
“Akina mama wengi tumekuwa wahanga wa maisha magumu, wanawake
tunahangaika sana kwani akina mama tunapoomba matumizi wanaume wanachukua
suruali na kuondoka bila kuaga,” alisema Mary.
Awali Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Geita, Neema Chozaile
alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili hali ya demokrasia nchini ambapo
alisema demokrasia inataka kupotezwa kwa kunyimwa uhuru wa habari, kujieleza na
kutoa maoni.
Alisema Serikali iliyopo ni ya kwanza kujitokeza kubinya
demokrasia nchini kwa kunyima uhuru hasa wa vyama vya siasa kujieleza kwa
wananchi.
0 comments:
Post a Comment