Mashaka Mgeta |
ADHIMISHO la pasaka linalowaunganisha
wakristu duniani kukumbuka safari ya mateso, kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristu
limefanyika kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Jana ilikuwa Jumatatu ya pasaka ambapo
waumini wa dini hiyo na watu wengine wenye mapenzi mema, wanaendelea kuishiriki
pasaka hadi itakapofika siku ya pentekoste.
Kwa mataifa yenye Serikali zisizotokana na
dini ikiwamo Tanzania, si rahisi sana kuhusisha matukio ya imani na mifumo ya
kawaida ya maisha ya watu na shughuli zao hususani siasa.
Lakini undani wa shughuli hizo ikiwamo
siasa zinatajwa katika namna inayolenga kuwapo na uongozi bora na mifumo
inayochangia watu kuwa na maisha bora ya duniani na mbinguni. Ndivyo
ilivyotokea katika pasaka, inavyotokea katika sherehe za Idd el Hajj, Eid
al-Fitr, krimasi na nyingine.
Viongozi wa dini wamekuwa wakitumia fursa
zinazotokana na sherehe ama maadhimisho hayo
kuwakumbusha watu namna bora ya kuishi na
kutenda, ama njia wanazopaswa kuzipita viongozi na watawala katika kuliongoza taifa
na watu wake.
Ndio maana viongozi kadhaa wa madhehebu ya
Kikristu waliitumia pasaka kuonya, kukaripia, kuelekeza na kufundisha,
wakijielekeza zaidi katika matukio ‘yanayoitetemesha’ nchi ikiwamo rushwa,
uhasama, ubadhirifu wa mali za umma, vitisho, dhuluma, utekaji, mauaji na uovu
mwingine.
Miongoni mwa viongozi hao ni Askofu
Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius
Nzigilwa anayeainisha maeneo matatu miongoni mwa mengi yanayopaswa kutafsiriwa
kama mafundisho ya pasaka kwa maisha ya watu.
Anayataja maeneo hayo kuwa ni wema dhidi
ya uovu ama ukweli dhidi ya uongo, upatanisho na maisha yenye matumaini mapya
ya kupata ukombozi. Anapoyataja maeneo hayo, unaweza kupata fikra za mafundisho
ya kiroho pekee.
Ingawa ni ukweli usiopingika kuhusu
mafundisho hayo kuwa ya kiroho, lakini yanagusa maisha ya watu pasipo kujali tofauti
za imani, itikadi ama vinginevyo, isipokuwa pale mhusika (Bwana Yesu) ‘anapotazamwa’
kwa namna tofauti.
Mhashamu Nzigilwa anasema, kwa mfano wa
kuundiwa mashtaka, kuteswa na kuuagwa, wakuu wa makuhani waliohofia kwamba
kutokana na kazi alizozifanya (Yesu) angeweza kuwaondoa katika madaraka yao.
Hawakujua kwamba utawala wake haukuwa wa dunia hii.
Lakini kiongozi huyo wa kiroho anasema
hata katika dunia ya sasa, wapo watawala wanaowaundia hujuma watu wema,
wakitaka kuwaangamiza ili kukidhi hofu zao na nia ya kulinda kuwapo kwao
madarakani.
Ushahidi wa fundishi hilo upo hata katika
siasa za nchi nyingi hususani barani Afrika. Viongozi kadhaa wa kisiasa
wamekuwa mfano wa waliojimilikisha tawala za kidunia, wakiunda njama na kutumia
ushahidi wa uongozi kuwaangamiza wanasiasa na raia wengine wasiokuwa na hatia.
Mhashamu Nzigilwa akasema haipaswi kwa
dunia kuwa mahali ambapo mtu asiyekuwa na hatia anaangamizwa ili kulipa maslahi
ya watu wengine. “Usipange uovu dhidi ya binadamu hata kipindi cha mpito,
utaona umeshinda, lakini elewa kwamba wema hauozi, ukweli utajulikana tu,” anasema.
Fundisho hilo linaweza kuwiana kwa karibu
na lile lililowahi kuasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,
likaingizwa kwenye ahadi za mwana-TANU, cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu
wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.
Inapotokea kiongozi akatumia cheo chake
ama cha mwingine kwa faida binafsi, ni rahisi kufungua mlango wa kupanga uovu dhidi
ya binadamu wengine.
Hivyo Mhashamu Nzigilwa anapolikemea hilo
katika sikukuu ya pasaka, anawakemea na wenye dhamana katika ngazi tofauti
wanaotumia vibaya madaraka yao dhidi ya wasiokuwa na hatia.
Mhashamu Nzigilwa anasema ipo haja kwa
watawala na wenye dhamana kutambua karama tofauti zilizopo kwa watu, kwamba zinapotumika
ipasavyo zinachangia katika ujenzi wa taifa.
Kwa upande mwingine, Mhashamu Nzigilwa
anasema pasaka inafundisha umuhimu wa upatanisho. Kwamba kama ambavyo Bwana
Yesu alirejesha upatanisho kati ya Mungu na wanadamu (kutokana na dhambi ya
asili waliyoitenda Adam na Hawa).
Mhashamu Nzigilwa akasema haifai kwa mtu
kufurahia mahangaiko ya binadamu mwingine na kwamba kinachopaswa kufanywa ni
kumsaidia ili aondokane na kadhia zinazomkabili.
Kwa bahati mbaya `dhambi’ ya kufurahia
mahangaiko ya watu imekuwa ikijikita katikati ya watu hata katika siasa, uongozi
na utawala. Imekuwa ni kawaida mtu kushangilia hata pale kiongozi ama mtu
mwenye dhamana anapotetereka katika kufanya uamuzi ama kutenda inavyostahili,
anapoutumikia umma.
Wapo wanaofurahia hata wale wanaopigania
haki za watu, wanaposhindwa kufikia malengo yao kutokana na dhuluma na hujuma wanazofanyiwa.
Ni ukweli ulio dhahiri kwamba upo upungufu
usiostahili kuvumilika, unaofanywa na viongozi ama watu wenye dhamana nyingine
kwa jamii. Upungufu huo unaweza kuwa katika ukweli halisi lakini unaokosa maana
pale ‘inapoongezwa chumvi’ ili kutimiza kusudio la kufurahia mahangaiko ya mtu
mwingine.
Kuondoka kwa hali kama hii kunaweza kuwa
na faidi nyingi ikiwamo kujenga na kuiimarisha misingi ya umoja na mshikamano
wa taifa na ‘kufunga milango’ dhidi ya maadui wa ndani na nje ya nchi.
Kwa hiyo taifa linalojijenga katika umoja,
linahitaji kuwa na mikakati ya kuwaleta pamoja ikiwamo kupitia njia ya
mapatano, ili kwa umoja wao washiriki katika kuilinda nchi, kujiletea maendeleo
na ustawi wa kila.
Hatimaye japo si kwa umuhimu, Mhashamu
Nzigilwa akataja kuhusu maisha ya matumaini mapya. Akasema kwa asili yake, mtu anapitia
njia mbalimbali katika vipindi vyake vya ukuaji. Anahangaika, anakumbwa na
shida na wakati mwingine kipindi cha raha. Ni sawa na ilivyo katika majira ya
siku kwamba kuna kipindi cha mvua na jua pia.
Inawezekana hali kama hizo zikatokea kwa
namna tofauti katika nchi inayopitia awamu tofauti za utawala kama ilivyo
Tanzania. Kwamba kulikuwa na awamu ya kwanza (Mwalimu Julius Nyerere), awamu ya
pili (Alhaj Ali Hassan Mwinyi) na awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Kisha ikaja awamu ya nne iliyoongozwa na
Rais mstaafu Jakaya Kikwete, akaikabidhi Ikulu kwa Rais John Magufuli aliyepo katika
awamu ya tano.
Katika vipindi ama awamu tofauti, yapo
mapito ya magumu ya maisha yanayowakabili watu, kiasi miongoni mwao wanakata tamaa.
Mhashamu Nzigilwa anazungumzia maisha ya matumaini mapya.
+255754691540
0 comments:
Post a Comment