Mwandishi Wetu
Mama Samia |
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan,
amesisitiza kuwa Tanzania ni moja ya nchi salama kwa uwekezaji Afrika.
Amesema hilo linasababishwa na kutokuwa
na matatizo ya migogoro ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa mali za
wawekezaji ikilinganishwa na nchi zingine Afrika.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jana
wakati akifungua maonesho ya kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania
yanayofanyika Dar es Salaam.
Pia alikaribisha wafanyabiashara na
wawekezaji wa Ufaransa kuwekeza katika maeneo mbalimbali hasa kwenye kilimo,
nishati, utalii na usafiri kutokana na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini.
Makamu wa Rais alisema maonesho hayo
ambayo yataambatana na kongamano la kibiashara la nchi hizo mbili ni fursa ya
kipekee kwa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa kubadilishana uzoefu katika
masuala ya kibiashara na uwekezaji.
Alieleza kuwa katika kuelekea kwenye
uchumi wa viwanda Tanzania haiwezi kufanya kazi hiyo peke yake, bali kwa
kushirikiana na mataifa makubwa yenye teknolojia ya kisasa katika uwekezaji
ikiwamo Ufaransa.
Aliwahakikishia wawekezaji wote
wanaokuja nchini kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana kuendelea kujenga
mazingira bora kwa ajili ya uwekezaji.
Alisema ili kuhakikisha Tanzania inakuwa
na mazingira bora ya uwekezaji Afrika, Serikali imeendelea kutenga bajeti ya
kutosha kuimarisha miundombinu ya bandari, reli, barabara, usafiri wa anga ili
kurahisisha usafiri na usafirishaji nchini.
Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak
alisema kongamano hilo litajikita katika kujadili kwa kina fursa za uwekezaji
nchini hasa kwenye nishati, usafirishaji, teknolojia ya habari na mawasiliano
na miradi ya maendeleo.
0 comments:
Post a Comment