Wankyo Gati, Arusha
UPANDE wa
Jamhuri umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kuiondoa kesi ya kujifanya Ofisa
Usalama wa Taifa (TISS) na kujipatia chakula kwenye hoteli moja ya kimataifa
jijini hapa, inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM)
wa Mkoa wa Arusha, Lengai ole Sabaya.
Akitoa maombi
hayo juzi, Wakili wa Serikali Grace Madikenya mbele ya Hakimu wa Mahakama ya
Hakimu Gwantwa Mwakuga, alisema upande wa Jamuhuri hauna nia ya kuendelea na
kesi hiyo kwa kuwa shahidi muhimu yuko nje ya nchi kwa miezi 18.
“Sasa tumeona
tutamtesa mteja wetu, hivyo kwa nia njema kabisa tumeamua kuiondoa mahakamani
kesi hii, maana miezi hii ni mwaka mmoja na miezi sita,” alisema.
Maombi hayo yalipingwa
na wakili wa utetezi, Edna Haraka na kuiomba Mahakama iendelee na kesi hiyo,
kwani upande wa mwendesha mashitaka unatumia Mahakama kama kichaka cha kumnyima
haki mteja wao na kumnyanyasa.
Alidai kuwa
upande huo hauna nia njema na mshitakiwa na kuiondoa kesi hiyo si mara ya
kwanza, ni mara ya pili, mara ya kwanza waliomba hivyo na Mahakama ilipoifuta
walimkamata mteja wao na kumnyima dhamana.
“Sasa leo tupo hapa
kusikiliza shahidi wa tatu na badala ya kuleta shahidi wanaleta maelezo ya shahidi
na stori ya kuiondoa ili waendelee kumnyanyasa mteja wetu, hapana ofisi ya Mwanasheria
Mkuu inatumika vibaya kwa kivuli cha Mahakama,” alisema.
Edna alisema Serikali
ya sasa inasisitiza mpango wa kuharakisha mashauri kusikiliza wa BRN, sasa
wakati inafanyika hivyo wengine wanachelewesha kwa sababu zao.
Hakimu Mwakuga
baada ya kusikiliza pande zote, alisema atatoa uamuzi Aprili 28.
Sabaya
anakabiliwa na mashitaka ya kujifanya Ofisa Usalama wa Taifa na kujipatia
huduma ya chakula na malazi kwenye hoteli ya kimataifa ya Highway jijini hapa.
0 comments:
Post a Comment