Suleiman Msuya
Freeman Mbowe |
KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni,
Freeman Mbowe amesema mwaka mmoja na nusu wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano
umekuwa ni wa manyanyaso na uonevu kwa baadhi ya viongozi na watendaji wao kuuwawa
au kupotea na Serikali ikiwa kimya.
Mbowe aliyasema hayo katika hotuba ya kambi
hiyo bungeni kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, mwishoni mwa wiki ambapo alitolea mfano
mauaji na kesi zinazowakumba wapinzani kila kukicha.
Alisema katika kipindi hicho wameshuhudia
mauji ya wanachama, kutekwa, kukamatwa kwa wabunge na wanachama na kesi
mbalimbali ambazo hazina msingi zikiwa na lengo la kuwakatisha tamaa.
Alitolea mfano kifo cha aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo na kusema aliuawa mchana
kweupe, huku watu wakishuhudia na kwamba waliohusika wanajulikana, lakini
hakuna hatua ambazo zilichukuliwa.
“Msaidizi wangu Ben Saanane alipotea
baada ya kupokea vitisho kadhaa vyenye asili ya kisiasa na hadi sasa vyombo vya
dola havijatoa maelezo ya kina ya Ben kapelekwa wapi,” alisema.
Mbowe alisema pamoja na changamoto hizo,
Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa upande wao na hila hizo za baadhi ya wenye
mamlaka, hazijawaondoa kwenye lengo kubwa la kuwavusha wananchi wa Tanzania
kuifikia ndoto zao.
Alisema wabunge wa upinzani hawajawa salama
kwa kile alichodai kuwa kifungo cha Mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali kilikuwa
cha uonevu mkubwa na Mbunge wa Arusha Godbless Lema kunyimwa dhamana kwa zaidi
ya miezi minne kwa shtaka lenye dhamana.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai
alisema katika kipindi hicho pia wameshuhudia Mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu akikamatwa mara kwa mara na vyombo vya dola na kufunguliwa mashtaka
mbalimbali yasiyo na nia njema wala afya kwa ujenzi wa demokrasia katika nchi
yetu.
“Tunaamini mapito haya mazito ya kisiasa
katika nchi yetu yanalenga kujaribu kufifisha ndoto ya Taifa ndoto
ya kuwa taifa huru linalosimamia misingi ya haki za binadamu, uhuru wa maoni ya
kila raia, demokrasia ya kweli, kuwa taifa linaloheshimu Katiba ya Nchi na
taifa lenye uchumi unaomnufaisha kila mwananchi,” alisema.
Mbowe alisema tangu Serikali ya Awamu ya
Tano iingie madarakani, zimeonekana dalili za wazi za Serikali hiyo kuvunja
Katiba ya Nchi kwa kutupilia mbali misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na
uhuru wa kupata habari jambo ambalo linaweza kuitumbukiza nchi yetu kwenye dola
la ki- dikteta.
Alibainisha matukio mahsusi ya
ukandamizaji wa haki na demokrasia yaliyofanywa na serikali kinyume cha Katiba
na Sheria za nchi kuwa ni pamoja na kupiga marufuku mikutano ya vyama vya
siasa.
Serikali kupitia Waziri Mkuu na Rais, ilitangaza
kwamba ni marufuku kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka
2020 ili kuipa Serikali nafasi ya kufanya kazi.
”Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya
Katiba aidha, katazo la mikutano ya siasa linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya
Siasa ya 1992 ambayo imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa,”
alisema.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema
kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa Mijadala ya Bunge ni kinyume na Ibara
ya 18 ya Katiba inayotoa uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kila
mwananchi.
Alisema pia bungeni yamekuwapo matukio
kadhaa yanayoashiria kutaka kuwadhibiti wabunge wa upinzani kwa lengo la
kuwanyamazisha wasiikosoe Serikali.
Kiongozi huyo alisema jambo hilo
limefanyika kwa namna mbalimbali, ikiwamo kuwazushia kesi wabunge wa upinzani
na kuwapeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambako hukumu
ya kuwaadhibu inakuwa imeshaandaliwa.
Alibainisha kuwa changamoto nyingine ni
Serikali kuingilia muhimili wa Mahakama, kupuuza utawala wa Sheria, uonevu
aliodai kufanywa na vyombo vya Dola dhidi ya Wananchi wa Visiwa vya Unguja na
Pemba.
0 comments:
Post a Comment