Grace Gurisha
ASKARI wawili
wanaotuhumiwa kuiba lita 280.6 za mafuta ya ndege wakiwa na watu wengine wawili
leo wanatarajiwa kupandishwa kizimbani mara ya pili kwenye Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi yao itakapotajwa.
Askari
hao ni F.8419 Koplo Bahati Msilimini (33), F.9901 Konstebo Benaus (34), na
wengine ni Iddy Nyangas (42) mlinzi wa kampuni ya Moko na Ramadhani Mwishehe
(52) fundi wa ndege, wote wakazi wa Dar es Salaam.
Watu hao
wanaoshitakiwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi wanatarajiwa kufikishwa mbele
ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Nassoro
Katuga atatakiwa kuiambia Mahakama hatua ya upelelezi ilipofikia.
Washitakiwa
hao wanadaiwa kutenda makosa mawili ya kula njama na hujuma wakiwa kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Ilidaiwa
katika mashitaka ya kwanza ya kula njama, kwamba katika tarehe tofauti kati ya Machi mosi na 17
mwaka huu, walikula njama ya kutenda kosa la hujuma.
Katuga
alidai katika mashitaka la pili kwamba, kati ya tarehe hizo wakiwa kwenye
uwanja huo, walifanya hujuma dhidi ya Serikali kwa kuhujumu maslahi ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Alidai
walitoboa na kuchota mafuta ya ndege lita 280.6 kutoka ndege namba 5H-MWF.DASH
8 Q 300. Baada ya kusomewa mashitaka, hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu
Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
“Hamtatakiwa
kujibu chochote kwa sababu makosa yenu ni ya uhujumu uchumi na pia Mkurugenzi
wa Mashitaka (DPP) hajawasilisha mahakamani hati ya kuitaka Mahakama hii
isikilize kesi hii,” alisema Nongwa.
Washitakiwa
wako nje kwa dhamana ya wadhamini wawili ya Sh milioni moja na pia walitakiwa
kutotoka nje ya nchi bila kibali pia kutosogelea eneo walilokuwa wakifanya kazi
bila kibali.
0 comments:
Post a Comment