Grace Gurisha
SERIKALI imewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kuwasafirisha Ali Hatibu Haji maarufu kama Shikuba na wenzake
wawili kwenda nchini Marekani kukabiliana na tuhuma za kujihusisha na dawa za
kulevya.
Maombi hayo yaliwasilishwa jana kwa nyakati tofauti na Wakili
wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki akishirikiana na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Veronika Matikila mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Cyprian Mkeha.
Kakolaki alidai kuwa maombi hayo yameanzishwa na Waziri
wa Katiba na Sheria na kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) alipatiwa
nakala kwa ajili ya kufuatilia, ambapo aliyawasilisha maombi hayo chini ya
sheria ya kusafirisha wahalifu na kuomba yasikilizwe kwa njia ya mdomo.
Alidai kuwa maombi hayo ni kwa ajili ya kuwakamata na
kuwasafirisha kwenda nchini Marekani wajibu maombi hao watatu kwa ajili ya
kujibu mashtaka ya kujihusisha na dawa za kulevya.
Aliwataja wanaotakiwa kusafirishwa kuwa ni Shikuba, Iddi Salehe
Mfuru na Tiko Emmanuel Adam. Pia aliomba Mahakama itoe amri ya kuwahifadhi
watuhumiwa wakati wa nasubiri kibali cha kuwasafirisha nje ya nchi kwenda kukabiliana
na mashtaka yanayowakabili.
Wakili wa Shikuba, Majura Magafu akishirikiana na Hudson
Ndusyepo alieleza kuwa wamesikia maombi ya upande wa mashtaka na akaomba wapewe
muda. Magafu alidai kuwa suala la kumtoa raia wa nchi yako nje ya nchi siyo
suala rahisi.
Kwa sababu walikwishafikishwa mbele ya mahakama aliomba
ahirisho ili waweze kupata nafasi ya kupitia makablasha waliyopewa.Alibainisha
kuwa makablasha hayo ni hati ya ushahidi ambao unatarajiwa kutolewa nje ya
nchi.
Hakimu Mkeha aliipanga kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kuyasikiliza
maombi hayo.
0 comments:
Post a Comment