Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imezuia usafirishaji mkaa kutoka wilaya moja hadi
nyingine katika hatua ya kudhibiti misitu isiendelee kuteketea nchini, huku
ikipiga marufuku usafirishaji mbao kutumia vivuli vya nyaraka za vibali.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akieleza kwamba mabadiliko hayo muhimu katika
biashara ya mkaa yataanza Julai.
Akifungua mkutano wa 24 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara
hiyo uliofanyika hapa, Profesa Maghembe alisema:
“Hakuna vibali vya kuhamisha mkaa kutoka wilaya moja
kwenda nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa ndani ya wilaya husika kwa ajili ya
matumizi ya Watanzania wanaohitaji nishati hiyo, lakini biashara ya mkaa ya
kutoa Dodoma kwenda Dar es Salaam hadi Zanzibar ni marufuku.”
Waziri alilalamika: “Wamekata misitu yetu yote, mito yetu
imekauka, tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji kwa sababu watu wengi huko nje
wanataka mkaa wetu.
“Tanzania si shamba la bibi, wote watakaotoa mkaa eneo
moja hadi lingine kinyume cha sheria watashughulikiwa kwa sheria ya uhujumu
uchumi.”
Alifafanua, kwamba kwa upande wa miji mikubwa kama Dar es
Salaam, Dodoma, Morogoro na Tanga, vitaanzishwa viwanda maalumu vya kuzalisha
mkaa ambao utauzwa kwa vibali maalumu mikoani.
Alisema mkaa huo hautakuwa na athari za kimazingira kwa
sababu utazingatia taratibu za uzalishaji endelevu.
Wakati huo huo, Waziri Maghembe alimwagiza Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kumhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Kikosi
cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu wa Wakala hiyo, Arjason Mloge.
Atatakiwa kutoka makao makuu ya Taasisi hiyo kwenda Chuo
cha Viwanda vya Misitu (FITI) mkoani Kilimanjaro na badala yake atafutwe mtu
mwingine mwaminifu.
Alisema uamuzi huo unatokana na udhaifu katika
usafirishaji wa rasilimali za misitu ndani na nje ya nchi, ukiwamo usafirishaji
kwa kutumia vivuli vya vibali haramu.
“Agizo hili litekelezwe mara moja kabla ya saa sita
mchana wa leo (jana) na niwe nimepewa nakala ya barua hiyo ya uhamisho,”
amesema.
Kwa uamuzi huo, alipiga marufuku kuanzia jana
usafirishaji mazao ya misitu ndani na nje ya nchi kwa kutumia vivuli hivyo.
Aliongeza kuwa katika kuunga mkono Sera ya Uchumi wa
Viwanda ya Serikali hakuna gogo litakalosafirishwa kwenda nje ya nchi.
Akizungumzia changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya
hifadhi nchini, alisema Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009
sehemu ya 21 (1) hairuhusu kuchunga mifugo kwenye hifadhi za Taifa, mapori ya
akiba, mapori tengefu na hifadhi za misitu.
Aliwataka watumishi wa Maliasili kusimamia sheria hiyo
pamoja na kutoa mwito kwa wananchi kuifuata kikamilifu.
Katika hatua nyingine, Waziri Maghembe aliwaonya
majangili kuacha biashara hiyo haramu
ambayo hailipi kwa sasa na badala yake wachukue trekta wakalime.
0 comments:
Post a Comment