Abdallah Amiri, Igunga
IGP Ernest Mangu |
KUNDI la watu zaidi ya 15 wanaosadikiwa
kuwa majambazi wenye mapanga, nondo na marungu wamefunga barabara na kuteka
madereva wa malori na maguta.
Tukio hilo lilitokea jana ambapo waliua
dereva wa guta na kumjeruhi wa lori huku wakiwapora fedha na simu kwenye kijiji
cha Igogo kata ya Nanga wilayani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa
shida akiwa amelazwa wodi namba nane katika hospitali ya wilaya, mmoja wa
madereva wa malori Ramadhani Bakari (34) mkazi wa Dar es Salaam, alisema alikuwa
akitoka Mwanza kwenda Iringa.
Alisema lakini baada ya kufika Igogo saa
6.30 usiku alikuta majambazi hao wametega magogo katikati ya barabara itokayo
Dar es Salaam kwenda Mwanza huku wakimwamuru ashuke.
Bakari alisema baada ya kushuka chini
majambazi hayo yalimwamuru atoe fedha na simu, na wakati anajiandaa kutoa fedha
majambazi hao walimshambulia kwa marungu na mapanga kichwani hali
iliyosababisha aanguke na kupoteza fahamu.
Bakari alibainisha kuwa baada ya kupata
fahamu, alijikuta yuko ndani ya gari lake huku milango imefungwa huku simu zake
mbili na Sh 40,000 zikiwa hazionekani.
Hata hivyo, Bakari alilishukuru Jeshi la
Polisi kwa kuwahi eneo hilo la Igogo
kwani majambazi hao walitumia dakika 20 kuteka magari na kuongeza kuwa kama polisi
wangechelewa majambazi hao wangefanya mauaji makubwa kwa madereva wa malori
kutokana na kipigo walichotoa.
Mmoja wa ndugu aliyeuawa ambaye
alijitambulisha kwa jina la Hassani alisema ndugu yake huyo, Charles Masanja alikuwa
akitoka kata ya Nkinga akiwa na magunia ya mkaa kwenye guta lake na alipofika
Igogo saa 6 usiku ndipo akakutana na masahibu hayo.
Akiwa na mwenzake, walikuta malori
yametekwa wakasimama lakini muda mfupi nao wakashambuliwa na kuporwa
Sh 300,000 huku Masanja akikatwa panga shingoni na
kupigwa nondo kichwani na polisi walipofika walimchukua yeye na mwenzake na
kuwakimbiza hospitali ya wilaya ambako muda mfupi alifariki dunia.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya,
Magongo Merchades alikiri kupokea majeruhi Masanja na Bakari saa nane usiku
huku akisema wakati wakipewa matibabu, Masanja alifariki dunia na kwa uchunguzi
wa awali, unaonesha kifo chake kilitokana na majeraha makubwa kichwani na
shingoni na kuongeza kuwa Bakari bado amelazwa wodi namba 8 na hali yake bado
ni mbaya.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, John Mwaipopo alithibitisha kutekwa
kwa madereva hao huku akifafanua kuwa maroli yaliyotekwa ni manne na kwamba
dereva wa guta kwa sasa ni marehemu kutokana na kujeruhiwa vibaya.
Aidha, Mwaipopo alisema hadi sasa Jeshi
la Polisi linaendelea na msako mkali dhidi ya majambazi hao na kuwataka
wananchi kutoa ushirikiano ili kukomesha vitendo kama hivyo visijirudie.
0 comments:
Post a Comment