Suleiman Msuya
BENKI ya Dunia imeitaja Tanzania kuwa
miongoni mwa nchi saba za Afrika Kusini mwa Sahara zinazoonyesha ukuaji wa juu
wa uchumi kwa mwaka 2015-2017.
Benki hiyo imesema nchi hizo zinazoendelea
zimeonyesha ustahimilivu wa kiuchumi, zikisaidiwa na mahitaji ya ndani ambapo
viwango vya ukuaji kwa uchumi wake kwa mwaka ni juu ya asilimia 5.4.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia
kwenye ripoti yake iliyotolewa jana kupitia Jarida la Africa Pulse, nchi
nyingine za ukanda huo zilizo na ukuaji uchumi unaofanana na Tanzania ni Ivory
Coast, Ethiopia, Kenya, Mali, Rwanda na Senegal.
“Wakati nchi zikielekea kwenye
marekebisho ya sera za fedha, tunahitaji kulinda mazingira sahihi ya uwekezaji
ili nchi za Afrika Kusini mwa Sahara ziweze kupata ukuaji imara,” alisema
Albert Zeufack, Mchumi Mkuu wa WB Kanda ya Afrika.
Jarida hilo limeenda mbali na kubainisha
kuwa uchumi wa nchi hizo unarudi katika kukua kuanzia mwaka 2017, baada anguko
baya zaidi kwa zaidi ya miongo miwili liliotokea mwaka 2016.
Ripoti ya jarida hilo ambalo huchapisha
uchambuzi wa hali ya uchumi mara mbili kwa mwaka kupitia Benki ya Dunia (WB)
ilisema nchi hizo zina takribani asilimia 27 ya idadi yote ya watu wa kanda na
zina asilimia 13 ya Pato Ghafi la Taifa la kanda.
Halikadhalika ripoti hiyo imebainisha
kuwa mwelekeo wa uchumi wa dunia unaboreka na utaweza kusaidia kurudisha ukuaji
katika kanda.
Jarida hilo linaeleza kwamba ukuaji
jumla wa bara unatarajiwa kupanda hadi asilimia 3.2 mwaka 2018 na asilimia 3.5
mwaka 2019, ukiakisi uchumi unaorejea kwenye hali ya kawaida katika chumi kubwa
zaidi.
Pia ripoti hiyo inabainisha kuwa ukuaji
uchumi utaendelea kuwa mdogo katika nchi zinazouza mafuta nje, wakati nchi
zinazouza madini za chuma zinatarajiwa kushuhudia ukuaji wa wastani.
“Ukuaji wa Pato Ghafi la Taifa katika
nchi ambazo chumi zake hazitegemei sana madini utaendelea kuwa imara,
ukisaidiwa na uwekezaji kwenye miundombinu, sekta za huduma stahimilivu, na
kufufuka kwa uzalishaji katika kilimo. Hali hii ni dhahiri kwa nchi za
Ethiopia, Senegal, na Tanzania,” ilisema taarifa.
Ripoti hiyo iliweka bayana kuwa kubana
zaidi kwa masharti ya fedha duniani kuliko ilivyotarajiwa, maboresho hafifu
katika bei za bidhaa na tishio linaloongezeka la sera za kulinda viwanda vya
ndani linalotokana na hisia za umma ni hatari zinazoweza kuukumba mwelekeo wa
kanda hiyo kiuchumi.
Ilisema kwa upande wa ndani, hatari
zinazoweza kuukumba hivyo kurudia ukuaji wa chini wa uchumi ni kasi ndogo ya
mageuzi, kuongezeka kwa vitisho vya
usalama na wasiwasi wa kisiasa kabla ya uchaguzi katika baadhi ya nchi.
“Tunahitaji kutekeleza mageuzi ambayo
yanaongeza tija ya wafanyakazi wa Kiafrika na kujenga mazingira tulivu ya
uchumi mkuu. Kazi bora zaidi na zilizo na tija ni muhimu katika kupambana na
umasikini katika bara,” alisema Zeufack.
Alisema mazingira ya ukuaji dhaifu wa
uchumi yanakuja wakati bara linahitaji sana kufanya mageuzi ambayo ni muhimu
kuinua uwekezaji na kupambana na umasikini.
Mchumi mkuu huyo alisema nchi zinatakiwa
kutekeleza maendeleo yanayohitaji fedha nyingi na wakati huo huo kuepuka
kuongeza deni la taifa hadi viwango visivyo endelevu.
Alisema katika mazingira hayo, kukuza
uwekezaji wa sekta za umma na binafsi, hususani katika miundombinu, ni
kipaumbele. “Kanda ilishuhudia mdororo katika ukuaji wa uwekezaji kutoka
takribani asilimia 8 mwaka 2014 hadi asilimia 0.6 mwaka 2015,” alisema.
“Wakati viwango vya umasikini vikiwa
vingali juu, kufufua kasi ya ukuaji ni muhimu,” anasema Punam Chuhan-Pole,
Mchumi Kiongozi wa Benki ya Dunia na mwandishi wa ripoti hii.
Alisema ukuaji unahitaji kujumuisha watu
wengi zaidi na utahusisha kukabilina na mdororo katika uwekezaji na gharama za
juu za kufanya biashara ambavyo vinazuia uwezo wa kushindana.
0 comments:
Post a Comment