Mwandishi Wetu, Chalinze
Miundombinu Barabara ya Buyuni |
MVUA kubwa iliyoambata na upepo mkali, imekata
mawasiliano ya miundombinu ya barabara Buyuni na kusababisha wakazi wa kata za
Vigwaza na Mwavi, kupata shida.
Hali hiyo imesababisha wakazi hao kuvushwa
kwa kubebwa migongoni kwa ujira wa kati ya Sh 2,000 na Sh 3,000 huku pikipiki zikitoza
Sh 5,000 kutokana na magari kushindwa
kupita kabisa.
“Mvua hapa bado haijanyesha, maji haya
yanatoka Msoga na kufika huku daraja la Mbiki, Buyuni na kukatiza katika hii
barabara, sipati picha mvua ikipiga hapa kwa mwezi huu itakuwaje,” alisema
Zaina Zuberi aliyekuwa njiani kwenda Mwavi.
Aliongeza: “Barabara ni mbovu kama
mnavyojionea, haipitiki, watu tunapata shida kufuata mahitaji ya nyumbani,
tatizo ni mkandarasi kwani barabara imejengwa bila makaravati, kila akielekezwa
kujenga kutokana na hali halisi ya barabara hafanyi hivyo.”
Baadhi ya vijana wanaosaidia kuvusha
watu na pikipiki walisema wabnafanya hivyo kwa makubaliano na wateja wao kwa
kuzingatia kipato tangu mvua zianze kunyesha Aprili 7.
“Tunapata fedha kulingana na kichwa cha
mtu au pikipiki, kila mtu Sh 3,000 au Sh 2,000 na pikipiki Sh 5,000,“ alisema
Rashid Juma.
Aidha, mvua hizo zimeathiri pia barabara
ya Milo-Kitonga-Vigwaza.
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alitembelea
barabara hizo na kujionea hali halisi.
Ridhiwani alisema hali iliyopo
hairidhishi na inawapa wakati mgumu wakazi wa maeneo hayo na aliahidi
kuisimamia kero hiyo kwa kuifikisha bungeni na Halmashauri ya Wilaya ya
Chalinze ili lifanyiwe kazi.
Alieleza kuwa kuna kila sababu ya
mkandarasi kufanya kazi kulingana na uhalisia wa eneo husika, hali
inayosababisha wananchi kupata tabu na barabara kuharibika kila wakati.
Katika hatua nyingine, Ridhiwani aliunga
mkono juhudi za ujenzi wa darasa lililobomoka kwa mvua iliyonyesha Aprili 7 na
alichangia Sh 100,000, mabati 50, mifuko ya saruji 50 na
nondo 20.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kaya zaidi
ya 20 zilikosa makazi na nyumba zaidi ya
90 zilibomoka na nyingine kuezuliwa mapaa jimboni Chalinze, kutokana na
mvua iliyoambatana na upepo mkali.
Maeneo yaliyokumbwa na adha hiyo ni
Chalinze Mzee, Bwawa la umwagiliaji la Msoga ambalo limefumuka na sekondari ya
Imperial.
0 comments:
Post a Comment