Is-haka Omar, Zanzibar
Dk Abdallah Juma Abdallah ‘Mabodi’ |
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah Juma Abdallah ‘Mabodi’, amesema
chama hicho kimejipanga kufanya siasa za ushindani wa kisera, kitaaluma, kibunifu
ili kwenda na wakati wa siasa za kisayansi zitakazojenga mazingira ya ushindi
wa Dola kwa CCM mwaka 2020.
Msimamo huo aliutoa juzi kwenye ziara
yake ya mwanzo tangu akabidhiwe madaraka iliyofanyika mkoa wa Kusini Unguja, akisema
chama kina nyenzo za kila aina zitakazotumika kwenye uwanja wa siasa ili
kuifuta CUF na vyama vingine vinavyoshirikiana na chama hicho katika historia
ya siasa za Zanzibar.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliweka wazi
kuwa atatumia falsafa ya Sayansi ya Siasa kufuta upinzani Zanzibar, kwani vyama
hivyo hasa CUF vimeshindwa hata kushauri utekelezaji wa Ilani ya CCM badala
yake vinaeneza chuki na misimamo ya utengano kwa wananchi.
Alisema vyama vyenye asili ya migogoro
na uchu wa madaraka, haviwezi kuongoza nchi, hivyo jamii iviepuke na wafuasi wa
vyama hivyo wahamie CCM kwani milango iko wazi ili wanufaike na siasa za
maendeleo na demokrasia imara.
Dk Juma alisema ili kufikia malengo hayo,
kila mwanachama na mfuasi wa CCM na wananchi kwa ujumla waendelee kuimarisha
dhana ya umoja na mshikamano huku wakitafakari njia bora za kuzibakiza
madarakani serikali za CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na wanachama wa tawi la Mtende mkoani humo aliwataka kufungua
ukurasa mpya kwa kuanzisha miradi ya maendeleo kwenye matawi yao, ili
wajitegemee badala ya kutegemea wabunge, wawakilishi na madiwani.
“Nakukumbusheni maendeleo yanayopatikana
hivi sasa yanatokana na radhi za wazee wetu waasisi wa ASP na TANU vilivyozaa
CCM inayotutengenezea maisha bora yanayoambatana na amani na utulivu kwa kila
mwananchi,” alibainisha.
Alitoa agizo kwa wabunge, wawakilishi na madiwani wa chama
hicho kuwasilisha mrejesho wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/20
kwa ngazi husika kila baada ya miezi mitatu, ili zifanyike tathimini za
kitaalamu zitakazopima utekelezaji.
Alihimiza kila tawi la CCM mkoa wa
Kusini kuwa na sanduku la maoni ili kila
mwanachama mwenye kero alitumie kuwasilisha maoni yake moja kwa moja ili Ofisi Kuu CCM Zanzibar ichambue kwa na
kubaini mambo yanayokwamisha utekelezaji
wa Ilani kwa baadhi ya maeneo.
Akizungumzia uchaguzi
wa chama unaoendelea ngazi ya matawi alisema chama bila wazee wenye
hekima na busara hakiwezi kwenda, kwani vijana peke yao hawana uwezo wa
kuongoza bila ushauri wao hivyo taasisi hiyo inahitaji mchanganyiko wa
makundi kugombea uongozi hasa ngazi za matawi.
Akishukuru, Mwakilishi wa Makunduchi,
Unguja, Haroun Ali Suleiman aliwambia wanachama kuendelea kuiamini na kuiunga
mkono CCM ili kuwaletea maendeleo endelevu huku ikilinda amani na utulivu wa
nchi.
0 comments:
Post a Comment