Mwandishi wa MAELEZO, Dodoma
Dk Hamis Kigwangalla |
SERIKALI imeanza hatua za awali za uainishaji gharama, uandaaji
mfumo mbadala na upembuzi wa kina wa aina ya ubia, ili kushirikiana na sekta
binafsi katika utoaji huduma za uchunguzi wa magonjwa.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kigwangalla, wakati akijibu hoja za
wabunge, Dodoma.
“Kutokana na kukua kwa kasi kwa Sayansi na Teknolojia ya
Uchunguzi wa Magonjwa, Wizara inakubaliana na wazo hili juu ya kuangalia namna
nzuri ya kushirikiana na sekta binafsi katika utoaji huduma hizi,” alisema
Kigwangalla.
Alisema kwa kuanzia sasa, Wizara yake inafikiria
kuanzisha ushirikiano kwa kupitia ukodishaji vifaa ambapo Serikali itakodisha
mashine hizo ambazo zitakuwa za mbia na Serikali haitahusika na ununuzi, ufungaji
na matengenezo kinga ya mashine hizo.
Alibainisha kuwa katika mfumo huo, Wizara yake itakuwa na
jukumu la kusimamia utoaji huduma na itapata gawio lake kutokana na makusanyo
yatokanayo na uchangiaji huduma kulingana na mkataba.
“Ni imani ya Wizara kuwa kutumia mfumo wa ubia na sekta
binafsi (PPP) huduma za uchunguzi wa magonjwa zitaimarika na kuipunguzia
Serikali mzigo wa gharama,” alisema Kigwangalla.
0 comments:
Post a Comment