Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta |
WANAFALSAFA na wanataaluma wengine waliobobea katika
masuala ya utawala, sayansi ya siasa na jamii wamewahi kutabiri, wakati
mwingine kuelekeza namna bora inayofaa kulijenga Taifa lenye mwelekeo wa kuleta
maisha bora na ustawi kwa watu wake.
Kwa mfano, mwandishi aliye raia wa Marekani, Toddy
Stocker katika tungo za semi mbalimbali, amewahi kuandika katika tafsiri isiyo
rasmi, uamuzi unaoufanya leo unaathiri matokeo ya kesho. Akimaanisha kila
kinachofanyika kwa muda uliopo, kina madhara, yawe hasi ama chanya kwa matokeo yajayo.
Stocker aliandika semi nyingi zenye maana na maudhui
tofauti. Semi zake hata sasa zinaendelea kuifundisha jamii pasipo kujali mipaka
ya kijiografia, hali ya uchumi, ukubwa na uimara wa jeshi kwa nchi husika ama
vinginevyo.
Inawezekana kukawapo tafsiri tofauti, lakini kwa mujibu
wa usemi niliouwasilisha ukiwa miongoni mwa semi nyingi, Stocker
anautahadharisha umma hasa watu wenye dhamana za uongozi, utawala, uwakilishi
ama dhamana yoyote yenye maslahi kwa umma, kuwa makini katika kujadili na
kufikia uamuzi.
Hoja ya Stocker inaweza kuwiana na falsafa ya Mgiriki wa
kale, Plato alipozitaja sifa za kiongozi (akimaanisha mtu mwenye dhamana ya
umma), kuwa ni pamoja na uwezo mkubwa wa kifikra katika kutafakari, kuchambua
na kufanya uamuzi sahihi kuhusu jambo lolote linaloihusu jamii anayoingoza.
Kwa maana nyingine, uamuzi unaofanywa na watu
waliokabidhiwa dhamana katika ngazi tofauti kwenye jamii, hata kuanzia familia
hadi taifa, wanaguswa na nadharia hizo na nyingine zinazoweza kutajwa na
zisitoshe kwenye ukurasa huu.
Kwamba kama Taifa, walio na dhamana kwa namna yoyote hapa
nchini, wanapaswa kuheshimu umuhimu wa misingi ya siasa na fikra za watu, ili
kuijenga jamii huru inayoshiriki katika kulijenga taifa.
Hivyo ‘leo’ ni wakati muhimu katika kuifanya ‘kesho’ ya
Taifa iwe katika hali gani. Iwe katika hali ambayo Mwanafalsafa Mtakatifu
Augustine wa Hippo katika karne ya tano, anaitaja kuwa ni ‘Jiji la Mungu’,
lenye utii, upendo, umoja, mshikamano na mengine yanayofanana na hayo.
Ama ‘kesho’ ya Tanzania itakuwa ‘Jiji la Jehanamu’ kwamba
inakuwa na watu wenye chuki, visa, uhasama, hujuma, ukosefu wa utii, vita na
aina nyingine za mafarakano yanayoharibu maendeleo na ustawi wa watu.
Ili kuwa mfano wa ‘Jiji la Mungu’, wenye dhamana
wanapaswa kuzitafakari na kuzifanyia kazi dhana za waandishi na wanafalsafa, japo
niliowataja hapo juu, ambao pamoja na wengine wengi maono yao yanaendelea
kuigusa hata jamii ya sasa.
Nimeyaandika kutokana na mfululizo wa matukio
yanayoikabili nchi. Ni matukio yaliyoshamiri zaidi baada ya kuanza kwa mfumowa
vyama vingi vya siasa, uliotanua wigo wa ufahamu wa watu kuhusu kushiriki
katika uongozi, uwakilishi ama kunufaika kutokana na fursa mbalimbali za
kidemokrasia na haki za binadamu.
Matukio ninayoyalenga hapa ni yenye kudhalilisha utu wa
mwanadamu, kukiuka haki za raia na vitisho vinavyoweza kuibua hofu miongoni mwa
watu, wakashindwa kutimiza wajibu wa kuijenga nchi inavyopaswa.
Matukio kama kushambulia, kujeruhi, kuua, kuteka na
kutisha kwa namna tofauti, hayakuzoeleka kwa Watanzania wanaosifika katika
kuendeleza misingi ya umoja, amani na utulivu vilivyoasisiwa na Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Viongozi hao ambao wote wametangulia mbele za haki
(Mwenyezi Mungu azidi kuwapumzisha katika usingizi wa amani-amina), waliiacha nchi
‘ikiwa moja’ licha ya kuwapo tofauti za mitazamo, itikadi na imani. Lakini hata
kabla ya kifo chake, dalili za kuondoka kwa hali hiyo zilianza kuonekana
zikiwamo ‘nyufa za Muungano’.
Miongoni mwa nyufa hizo ni ubaguzi ambao Mwalimu Nyerere
alisema kama utaachwa uendelee, wabaguzi wakimaliza kuwabagua wenzao watarejea
na kujibagua wenyewe. Madhara yake ni mafarakano.
Kwa muda mrefu sasa, mathalani wanasiasa hasa wa upinzani
wamekuwa wakilalamika kutotendewa haki na watawala. Walilalamikia kunyanyaswa,
kudhalilishwa, kubaguliwa, kuhujumiwa, kupata kejeli na kunyimwa haki za kidemokrasia.
Walilalamikia kunyanyaswa hasa waliposhiriki matukio kama
mikutano ya hadhara, walidai kudhalilishwa ndani na Bunge na kupitia vyombo vya
Dola kama ilivyokuwa kwa kadhia nyingine dhidi yao.
Miongoni mwao wakasema, malalamiko yao hayapaswi kupuuzwa
kwa maana yanaweza kutoka kwao yakaelekezwa kwa kada nyingine, na baadaye
kuingia katika mifumo wa nchi na hivyo kuifanya isiwe mahali rafiki kwa maisha
ya watu.
Vilio vya wapinzani vilipozidi huku vikipingwa kwa hoja
za watawala, vikazoeleka na kuonekana kuwa vya kawaida. Lakini hawakuchoka, waliendelea
kulalamika.
Vitendo walivyofanyiwa wapinzani ama baadhi yake
vikadaiwa kufanywa kwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga, ingawa
kwenye maeneo yao ya biashara. Vikaenea kwa waandishi wa habari na kada
nyingine. Idadi ya wanaolalamika ikazidi kuongezeka.
Pamoja na matukio hayo, ndani ya vyama vya siasa
kukaibuka vikundi vilivyopewa mafunzo yaliyobatizwa ‘ulinzi wa chama’. CCM
wakawa na Green Guards, Chadema wakakijenga Blue Guards wakati CUF ikiwa na Red
Brigade.
Vikundi hivi kwa namna tofauti vikatuhumiwa kushiriki
mafunzo ya kujihami, kupiga na kujeruhi, lengo likiwa ni kutimiza malengo ya kisiasa
yaliyo nje ya maslahi ya umma.
Wapo watu waliopigwa hasa nyakati za uchaguzi mdogo.
Ilitokea Tarime, Igunga na Arumeru Mashariki. Wapo waliolalamika kwamba
mwenendo wa vikundi hivyo haukuwa wenye kulielekeza Taifa katika misingi yake
iliyojikita katika utu, umoja na mshikamano. Walioasisi walipuuza, wakanyamaza,
wakaviendeleza ama kusaidia jitihada za kuviendeleza.
Ikaelezwa kwamba waliopewa mafunzo walipohitimu
wakatimiza wajibu wao, japo kwa uchache wao kutokana na ufinyu wa kazi
zilipojitokeza. Kuna taarifa kwamba kila kwa nafasi yake hakijui baadhi ya
‘walinzi’ waliopitia mafunzo kwenye vikundi hivyo hivi sasa wapo wapi.
Katikati ya hali hiyo, kunaibuka hulka ya kuteka watu,
kuwatesa na kuwajeruhi. Yalishatokea kwa wanasiasa kama waliokuwa Mwakilishi wa
Mkunazini, Salum Msabaha, kiongozi wa Chama cha Madaktari, Dk Steven Ulimboka,
Mhariri wa gazeti la Mtanzania, Absalom Kibanda na hivi karibuni mwanamuzi wa
kizazi kipya, Ibrahim Musa maarufu kama Roma Mkatoliki.
Wapo wengine waliowahi kukumbwa na kadhia kama
zilizowakabili hao, hata kama taarifa zao hazikuandikwa, lakini ukweli unabaki
kuwa ni matukio yasiyoistahili Tanzania na Watanzania.
Lakini kubwa zaidi ni kutishiwa kwa bastola kwa aliyekuwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, muda mfupi baada ya
Rais John Magufuli kutangaza kumvua wadhifa huo.
Nape alikumbwa na kadhia hiyo aliposhuka kutoka kwenye
gari lenye namba za Serikali, ikiashiria alikuwa bado hajakabidhi ofisi na mali
za ofisi.
Yapo matukio mengi ambayo hayajaibuka ghafla.
Yaliandaliwa, yakapikwa, yakatekelezwa katika vipindi tofauti na sasa
yanaelekea kujikita kwenye mioyo na makusudi ya baadhi ya watu. Nchi inakwenda
katika mwelekeo ambao haukuwapo awali.
Tunapolikumbuka onyo la Mwalimu Nyerere, kwamba
‘mkimaliza kuwabagua wale, mtajibagua ninyi wenyewe’ kadhalika vitendo
vinavyotenegenzwa leo dhidi ya raia halali wa Taifa hili, vitaliathiri taifa katika
siku ijayo ama zinazokuja.
Vitendo hivyo vinaweza kuwa vilivyohusishwa kwenye Makala
haya, japo kwa mfano, ama vile vya hujuma za kisiasa.
Ni lazima kila raia pasipo kujali nafasi yake kwenye
jamii, atambua kwamba kila kinachotengenezwa leo kina athari kwa nchi. Ni vema
zikawa athari chanya zinazotokana na matendo ya jana, nchi itasonga mbele.
+255754691540
0 comments:
Post a Comment