Jemah Makamba
MKAZI wa Buguruni Dar es Salaam, Fatuma
Yusufu (40) amehukumiwa kwenda jela miaka miwili baada ya kupatikana na hatia
ya wizi wa Sh milioni mbili mali ya Natoza Haule.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu
Benjamin Mwakasonda wa Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo, alisema Mahakama ilijiridhisha
na ushahidi dhidi ya mlalamikiwa na kumtia hatiani.
Hakimu alisema ushahidi uliotolewa na mlalamikaji
ambaye ndiye alikuwa shahidi namba moja katika kesi hiyo, ulithibitisha namna alivyoiba
fedha hizo.
Awali shahidi alidai mahakamani hapo
kwamba siku ya tukio, akiwa mfanyakazi wa usafi katika Chuo cha Biashara (CBE)
Dar es Salaam, alifika wa kwanza asubuhi na kumwomba mlinzi ufunguo ili aanze usafi.
Alidai kuwa baada ya kufika ofisini
mwake alikuta droo yake imevunjwa na fedha alizokuwa ameacha zimetoweka.
Shahidi huyo alidai kuwa baada ya hapo
alimtafuta mlinzi na kumhoji nani alikuwa wa kwanza kuingia akaambiwa ni mtu wa
usafi ambaye ni mshitakiwa na alikuwa ameondoka eneo hilo na hakutokea hadi
alipokamatwa.
Kutokana na ushahidi huo, mshitakiwa alikutwa
na kesi ya kujibu na Mahakama kumtia hatiani kwa wizi.
Hakimu alimwuliza Karani, Saidi Benea
kama kuna kumbukukumbu za makosa ya nyuma ya mshitakiwa akasema hakuna ila mshitakiwa
apewe adhabu kali iwe fundisho.
Mshtakiwa aliulizwa na Hakimu kama kuna
chochote cha kuiambia Mahakama kabla ya kupewa adhabu.
"Hakimu mimi ni mgonjwa, naumwa na
natumia dozi lakini pia mama yangu mzazi ni mzee sana, mimi ndiye namtunza
naomba huruma yako," mshitakiwa aliomba.
Maombi hayo hayakumzuia Hakimu kutoa
adhabu hiyo, ya kwenda jela miezi 24 na akitoka alipe fedha hizo.
0 comments:
Post a Comment