Suleiman Msuya
Bella Bird |
BENKI ya Dunia (WB), leo itazindua ripoti
ya tisa ya hali ya uchumi nchini katika hafla itakayofanyika Dar es Salaam.
Taarifa ya benki hiyo kwa vyombo vya
habari kupitia Ofisa Mawasiliano wake, Loy Nabeta jana, ilieleza kuwa Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia (WB), Bella Bird, atazindua ripoti hiyo huku Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji akiwa mgeni rasmi.
Nabeta alisema WB imekuwa na utaratibu
wa kutoa ripoti ya uchumi kwa nchi wanachama, Tanzania ikiwa moja wapo.
Alisema wadau watashiriki kuijadili
ikiwa ni pamoja na kupitia sera mbalimbali ambapo kwa pamoja watakuja na maoni
ya hali ya uchumi nchini.
Ofisa Mawasiliano huyo alisema kila
ripoti inayotolewa imekuwa ikijadili sekta husika kwa kina ambapo kwa hii itajikita
zaidi kuonesha mchango wa sekta ya fedha nchini.
“Katika uzinduzi huo pamoja na
Mkurugenzi Mkazi wa WB pia watakuwapo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Profesa Benno Ndulu, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker, Mshauri
Mwandamizi wa Kampuni ya Ushauri ya Rex, Dk Hawa Sinare, Mhadhiri Mwandamizi wa
Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Maxcom
Afrika, Ahmed Lussasi.
Wakati ripoti hiyo ya uchumi ikitarajiwa
kuzinduliwa leo ripoti ya mwaka jana inaonesha uchumi wa Tanzania Mei mwaka
jana ulikua kwa asilimia 6-7.
Ripoti ya mwaka jana ilionesha mfumuko
wa bei ulikuwa unapungua kuanzia Januari kutoka na ununuzi mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment