Celina Mathew
Frederick Sumaye |
ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Frederick Sumaye,
amesema kushuka kwa kiwango cha biashara nchini kunatokana na usimamizi mbovu
wa sera za uchumi.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam hivi
karibuni ambapo alisea usimamizi mbovu ni pamoja na mfumo mbovu wa ukusanyaji mapato,
ambao unawafanya wahusika kuona wanatozwa kodi kubwa kuliko wanayoweza kulipa.
“Hivi karibuni tumeshuhudia kampuni
nyingi zikifungwa na nyingine kupunguza wafanyakazi kutokana na kudorora kwa
biashara tofauti na miaka iliyopita hali inayosababisha ugumu wa maisha na
malalamiko,” alisema.
Alitaja masuala mengine yanayotishia
biashara kuwa ni pamoja na vitisho mbalimbali kutoka vyombo vya dola na ukiukwaji
wa mikataba.
“Kwa kiasi kikubwa kampuni zinaweza
kupunguza wafanyakazi kutokana na uchumi mbovu au usimamizi mbovu wa sera za
uchumi,” alisema Sumaye.
Alisema kwa kiasi kikubwa kampuni za
biashara au biashara yoyote lengo lake kuu ni kutengeneza faida ambayo
itatokana na biashara inayofanyika.
Aliongeza kuwa kama kiwango cha biashara
kitapungua, mfanyabiashara atapunguza gharama za biashara ambayo ni
pamoja na watumishi au kufunga kabisa biashara hiyo, ili isizidi kumletea
hasara.
Alipoulizwa ni nini yalikuwa makosa
wakati wa uongozi wa Rais Benjemin Mkapa alisema kuwa Serikali zote huendeshwa
na binadamu na siyo malaika.
“Hivyo lazima kuna mambo mema na makosa
ambayo kila serikali hufanya. Muhimu ni kuwa yasiwe makosa ya makusudi bali ya
utendaji ambayo yanarekebika. Wako wanaosema uuzaji wa mashirika ya umma
ulikuwa makosa,”alisema na kuongeza.
“Mimi nasema siyo makosa kwani ilikuwa
sera ya chama tawala ambayo Serikali na Bunge viliipitisha. Hata hivyo
tukumbuke mengi ya mashirika hayo yalikuwa yamefilisika hata kulipa mishahara
ya watumishi ilikuwa hailipwi kwa muda mrefu.”
0 comments:
Post a Comment