*Wadaiwa kuvamia kwa silaha mkutano wa wanahabari
*Mutungi aonya wanachama waheshimu kesi
ya utata
Abraham Ntambara
Kamansa Simon Siro |
SAA tatu baada ya viongozi wa CUF
kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro,
kuhoji sababu za kutokamatwa watu waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi
wa habari na viongozi wa chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi
limetangaza kushikilia watu watano.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi
ya Chama hicho Julius Mtatiro, viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni
ajabu kuona Polisi haijachukua hatua huku
ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi wanahabari na viongozi wa chama hicho
katika tukio ambalo liliripotiwa na vyombo vya habari.
Viongozi hao walikutana na Sirro jana saa
5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda
huyo alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao,
wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo.
Jumamosi iliyopita takribani watu watano
wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo
uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya
vurugu.
Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa
amejifunika uso kininja alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa
kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire
na kumshushia kipigo.
Katika ufafanuzi wake, Mtatiro alisema
tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho,
Maalim Seif Sharif Hamad lakini vyombo vya Dola viko kimya.
“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa
kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya
tu,” alisema Mtatiro.
Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo,
alisema: “Tulitaka kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko
wapi. Mvamizi mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na
kuokolewa. Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”
Alisema baada ya tukio hilo, Mkuu wa
Upelelezi aliwapigia simu viongozi waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni wakapatanishwe.
“Tulishangazwa na taarifa hiyo, kwa watu
waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha
watu wenye makosa ya jinai, kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa
mahakamani,” alisema Mtatiro.
Alisema sababu nyingine ya kwenda
kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya
sheria.
“Tulimwonya Kamanda Sirro kwamba sisi
(upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba na kuiomba Polisi kutekeleza
majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya wavamizi hao,” alisema.
Sirro
Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro
alisema Polisi inashikilia watu watano wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye
mkutano huo.
“Tulipata taarifa ya kuvamiwa kwa
mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya
taarifa hizo kupokewa askari walifuatilia na kukamata watu watano,” alisema
Sirro.
Alisema watuhumiwa hao wanaendelea
kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.
Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na
kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.
Msajili aonya
Pamoja na CUF upande wa Katibu Mkuu,
Maalim Seif Sharif Hamad ikimtuhumu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi kwa kuchochea mgogoro unaoikabili, mwenyewe amewataka wanachama hicho
kuheshimu kesi ya utata wa uongozi inayoendelea mahakamani.
Kupitia taarifa yake yenye kichwa cha
habari ‘Kulaani vurugu zilizotokea katika mkutano wa wanaosemekana kuwa viongozi
wa CUF na waandishi wa habari’, Jaji Mutungi alisema uwepo wa kesi mahakamani
hauwapi mamlaka wanachama hao kufanya vurugu.
“Ninaviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa
haviko juu ya sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata sheria za nchi, ikiwamo
kutunza amani na utulivu tulionao,” alisema.
Kauli ya Jaji Mutungi imekuja siku mbili
tangu watu waliotumia gari lilikokuwa na nembo na bendera za CUF, kuvamia
mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na viongozi wa chama hicho wilaya
ya Kinondoni.
Katika tukio hilo, watu hao walipiga
wanahabari na viongozi hao huku mmoja wa wavamizi aliyejifunika uso kininja,
akichomoa bastola kutishia na mwingine akishindwa kuondoka na kushushiwa kipigo
na wananchi.
Juzi upande wa Maalim Seif ulimtuhumu
Mwenyekiti wa Chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuhusika na vurugu hizo, tuhuma ambazo
zilikanushwa na wanaomuunga mkono.
Katika maelezo yake, Jaji Mutungi
alisemaa suala la mgogoro wa uongozi katika CUF liko mahakamani, hivyo akiwa
msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na mlezi wa vyama hivyo anakisihi chama
hicho kutambua kuwa uwepo wa shauri mahakamani, si fursa ya kufanya uvunjifu wa
amani.
“Jambo hili ni uvunjifu wa sheria na
linaleta sura mbaya kwa jamii. Ninalaani vurugu hizo ambazo zilionekana kuvunja
amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na
utulivu,” alisema.
“Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na
tofauti walizonazo, madhali masuala haya yako mahakamani, hebu tuheshimu
utawala wa sharia,” alisema.
Alisema ofisi yake na Jeshi la Polisi
wanashughulikia malalamiko yoyote kuhusu uendeshaji na shughuli za chama
chochote cha siasa, hivyo hakuna haja ya wanachama wa CUF kukiuka taratibu za
kuendesha chama hicho na kujichukulia sheria mkononi.
Jaji Mutungi alivitaka vyombo vya ulinzi
na usalama nchini kufanyia kazi tukio hilo ili wahusika wafahamike na
kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
inayosimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, haitasita kuchukua hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.
0 comments:
Post a Comment