Leonce Zimbandu
Hebron Mwakagenda |
JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limetaka taarifa rasmi
itolewe kwenye Gazeti la Serikali kwamba mchakato wa Katiba mpya uko hai na
unaendelea ili kupata Katiba Mpya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alitoa
tamko hilo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.
Tamko hilo limekuja siku chache baada ya Waziri wa Katiba
na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, kuzungumza na wajumbe wa Kamati ya Bunge
ya Sheria na Katiba na kuwaeleza kwamba Serikali itaanza kurekebisha sheria ili
kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.
Lakini Mwakagenda alisema kabla ya marekebisho ya sheria
kuwasilishwa bungeni, itakuwa busara wadau kuyapitia ili kukubaliana eneo ambalo
mchakato unapaswa kuanzia na kuepusha mpasuko wa kitaifa.
“Tunafahamu kuwa Profesa Kabudi ni nguli katika masuala ya
sheria, hivyo atakuwa daraja la kufanikisha mchakato wa Katiba na hatimaye
kupata mpya,” alisema.
Alisema tangu kuanzishwa kwa mchakato huo, wamepita
mawaziri watatu na Profesa Kabudi atakuwa wa nne, alianza marehemu Celina
Kombani, Mathias Chikawe na Dk Harrison Mwakyembe.
Alisema kutoka na weledi alionao Waziri, anapaswa
kuwasilisha mswada wa marekebisho wa sheria ili kurekebisha sheria iliyosimamisha
mchakato, huku Serikali ikijipanga kuipangia bajeti.
Mjumbe wa Bodi ya Jukata, Mpendwa Chihimba alipongeza
hatua ya Profesa Kabudi ya kutaka Serikali ianze kufanya marekebisho ya sheria
ili mchakato uanze.
Alisema hatua hiyo inapaswa kupongeza kwani haiwezekani Waziri
azungumze na Kamati ya Bunge bila kuzungumza na kushauriana na Rais John
Magufuli.
“Watanzania tuonde hofu, mchakato wa Katiba umo mbioni,
hivyo hakuna sababu ya kukata tamaa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment