Mwandishi Wetu
Dk. Hamisi Kigwangalla |
NAIBU Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na
Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla amehimiza watumishi wa Wizara yake kuacha kufanya
kazi kwa mazoea na kuzingatia sheria, miongozo, taratibu na maelekezo ya kazi.
Akiwa kwenye ziara ya Mtwara, juzi alielekeza watumishi hao
kuwa dhamana waliyopewa kuhudumia wananchi wenzao ni kubwa, hivyo hawana budi
kuzingatia kanuni za afya ili kuepuka maambukizi yatakayotokana na uzembe.
Aliwataka kulipa kipaumbele suala la usafi wa mazingira,
vifaa na maeneo yote wanayofanyia kazi hususan uhifadhi wa taka za hospitali
katika utaratibu maalumu unaozingatia mfumo wa kinga na udhibiti wa taka.
Miongoni mwa mambo aliyobaini katika ziara hiyo ni ubovu
wa baadhi ya vifaa tiba katika maabara na vyumba vya upasuaji na kuagiza Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, kuchunguza mikataba yote ya usambazaji vifaa tiba na
matengenezo.
Aidha, Dk Kigwangalla alibaini baadhi ya vifaa vya kisasa
vilivyo kwenye vituo hivyo havitumiki ipasavyo, kwa sababu watumishi waliopo
hawana ujuzi wa kuvitumia na alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kulishughulikia
tatizo hilo haraka kwa kuwajengea uwezo wataalamu hao.
Mbali na kujionea hali hiyo, Dk Kigwangalla pia alitoa
maagizo kwa watendaji wa vituo na viongozi wa wilaya husika kuhakikisha
wanasimamia ipasavyo utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Dk Kigwangalla akiwa Mtwara, alitembelea zahanati, vituo
vya afya na hospitali, kati hizo kuwa ni: Kituo cha Afya Mahurunga, cha Nanguruwe
na zahanati ya kijiji cha Dinyecha.
Pia alitembelea Hospitali ya Wilaya ya Newala na Kituo
cha Afya cha Newala DC, zahanati ya Lulindi, ya Nagaga, hospitali ya Halmashauri
ya Masasi-Mkomaindo na zahanati ya Mbonde.
Aidha, aliendelea na ziara yake Ruvuma ambako atatatembelea
vituo vya afya na hospitali za mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment