Mwandishi Wetu
KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini, Profesa James Mdoe amefanya mazungumzo na uongozi wa kampuni za
Uranium One na Mantra Tanzania wanaomiliki leseni ya uchimbaji madini ya urani kwenye eneo la Mto Mkuju Kusini mwa nchi.
Mantra ni sehemu ya kampuni ya Uranium One na
kampuni ya kimataifa ya madini ya ROSATOM-ya Shirikisho la Serikali ya Urusi ya
Nishati ya Nyuklia.
Kikao hicho kilijadili ushirikiano kati ya Tanzania
na kampuni hizo, kuporomoka kwa bei ya urani kwenye soko la dunia na kampuni
hizo kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika miradi ya
madini.
Rais wa Uranium One Group, Vasility Konstantinov
aliishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoendelea kuutoa kwao ili kuhakikisha
kuwa lengo la kampuni la kuendeleza mradi wa uchimbaji madini ya urani nchini linafanikiwa.
Konstantinov pia alikanusha habari zilizoandikwa na
baadhi ya magazeti nchini hivi karibuni kuwa MANTRA
Tanzania imesitisha uchimbaji wa urani kwenye leseni yao iliyoko eneo la Mto
Mkuju moja ya sababu ikiwa ni mabadiliko katika Sheria ya Madini.
Alisisitiza kuwa maombi ya Mantra
Tanzania ya kupata ridhaa ili kusitisha
uchimbaji madini ya urani kwa muda wa miaka mitano, yanatokana na kushuka kwa
soko la madini duniani na kwamba suala hilo halijaiathiri kampuni hiyo pekee,
bali hata baadhi ya kampuni.
“Mradi huu ni muhimu kwa ROSATOM,
hatutaki kuondoka, tunataka kuendelea kuwa hapa, tuendeleze ushirikiano mpaka
hapo bei ya urani itakapopanda ili tutekeleze mradi kwa manufaa ya pande zote
mbili,” alisema Konstantinov.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea
kuendeleza miradi mingine ya kijamii mkoani Ruvuma, na tayari wamejadiliana na
uongozi wa mkoa kuona jinsi watakavyoshiriki kwenye miradi hiyo ya kijamii.
“Hii inaonesha kuwa mradi huu ni muhimu
kwetu na tunataka kuuendeleza mapema iwezekavyo, lakini kikwazo sasa ni
kuporomoka kwa bei ya urani,” alisema Konstantinov.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania,
Frederick Kibodya alisema uwasilishaji wa maombi ya kusitisha uchimbaji
urani serikalini, haumaanishi kuwa kampuni hiyo itasimamisha shughuli zake zote
nchini.
Alisema kampuni hiyo itaendelea
kufadhili miradi ya kijamii na imeanza mazungumzo na STAMICO ili kushirikiana kuendeleza
miradi ya uzalishaji makaa ya mawe na dhahabu.
Profesa Mdoe aliwaeleza watendaji wa
kampuni hizo kuwa maombi yao la usitishaji uchimbaji madini ya urani nchini yamefika
serikalini na kwamba yatatolewa uamuzi muda mwafaka ukifika.
Kuhusu nia ya kampuni hiyo kushirikiana
na STAMICO kwenye miradi ya madini,
Profesa Mdoe aliikaribisha kwani lengo la Serikali ni kukaribisha wawekezaji
nchini wenye nia njema ya kuendeleza miradi itakayoleta tija kwa Taifa.
Kuhusu mabadiliko katika Sheria ya
Madini, Profesa Mdoe alisema lengo ni kuhakikisha nchi inafaidika na rasilimali
zake na kama mwekezaji anafuata matwaka ya nchi katika uwekezaji, atakuwa hana
sababu ya kuogopa mabadiliko.
“Mabadiliko ya Sheria ya Madini ni kwa
ajili ya kunufaisha pande zote na si kunyanyasa
mwekezaji, kama mwekezaji anakuja kwa nia nzuri hana sababu ya kuogopa,”
alisema Profesa Mdoe.
0 comments:
Post a Comment