Mwandishi Wetu
Waziri Angella Kairuki |
SERIKALI imejiweka katika hatari ya
kudaiwa mabilioni ya fidia na watumishi wa umma 450 waliobainika kutangazwa
kimakosa kuwa wamiliki wa vyeti feki.
Wakizungumza na mwandishi wa JAMBO LEO
kwa masharti ya kutotajwa gazetini jana, baadhi ya wanasheria waliweka wazi
kuwa ni haki kwa watu hao kuishitaki Serikali kwa mujibu wa sheria ya kudai
fidia baada ya kukashifiwa.
Mmoja wa wanasheria hao alisema inafahamika
kuwa mtu anayefanyiwa hivyo na baadaye kubainika kuwa haikuwa hivyo, anapata
athari.
“Hilo jambo liko wazi na hata Serikali
inafahamu kuwa haki ya kushitaki, mtumishi anayo labda kama wataogopa kuishitaki
Serikali ambayo inawalipa mshahara,” alisema.
Mwanasheria mwingine alisema kumwita mtu
ana cheti feki ni kumdhalilisha, lakini kwa kuwa imethibitika vinginevyo,
mwajiri ambaye ni Serikali, anapaswa kumrudisha kazini na kumpa stahiki zake
zote.
“Huyo anatakiwa arudishwe kazini na kama
mwajiri wake ataona hayupo tayari kufanya hivyo, anatakiwa ampe stahiki zake
zote na huo ndio utaratibu kisheria.
“Anaweza kushitaki kwa kudhalilishwa,
lakini hata akishitaki mwajiri atatakiwa kumrudisha kazini na kama hataki
kuendelea kufanya naye kazi, anatakiwa kumlipa stahiki zake zote kutokana na
kumchafulia jina,” alisema mwanasheria huyo.
Juzi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma Utawala Bora, Dk Laurian Ndumbaro alisema awali
watumishi wa umma 9,932 walibainika kukutwa na vyeti feki, katika
uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu uliofanywa na Serikali.
Alisema baada ya kutangazwa kwa orodha ya
watumishi hao, watumishi 1,050 walikata rufaa na baada ya kupitia rufaa hizo, watumishi
450 walishinda rufaa hizo.
Alifafanua kuwa katika rufaa
zilizokubaliwa, ilibainika kuwa baadhi ya watumishi walikuwa wakitumia majina
ya waume zao baada ya kuolewa, ambayo yalitofautiana na majina yaliyo kwenye
vyeti.
“Bahati mbaya Watanzania wanapoolewa hutumia
majina mawili ya waume zao, badala ya moja. Hivyo ilileta usumbufu wakati wa
uhakiki baada ya vyeti vyao kuonesha majina tofauti,” alisema.
Wengine walioshinda rufaa ni ambao majina
yao ya kidato cha nne, yalikuwa tofauti na ya kidato cha sita, kwa kuwa kidato
cha nne hawakutumia majina ya kati kama ya kidato cha sita, lakini baada ya
kujieleza walikubaliwa rufaa na kurejeshwa kwenye utumishi wa umma.
Wengine ni walioonekana kuwa na karatasi
za vyeti ambazo si sahihi, lakini matokeo ni sahihi na walisoma kwenye shule
husika na baada ya kuhojiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), walionekana
walipata vyeti shuleni kwao, lakini karatasi zilizotumika hazikuwa sahihi
kutokana na wao kuchelewa kuchukua vyeti vyao kwa miaka mingi.
“Hawa wa kundi hili hawakuwa na lengo la
kubadilisha matokeo, hivyo ilionekana wanastahili kurejeshwa kwenye
utumishi wa umma, kwa kuwa walipewa vyeti ambavyo havikubadilishwa matokeo,” aliongeza.
0 comments:
Post a Comment