Mwandishi Wetu
SERIKALI imeagiza uongozi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kupitia upya mikataba minne ya
watoa huduma kwenye uwanja huo, kutokana na kugubikwa na utata huku ikisisitiza
kubadilisha uongozi huo.
Pia imesisitiza kuwa wiki ijayo itaunda
timu ya wataalamu wa kupitia mikataba hiyo minne, pamoja na mingine inayohusu
uwanja huo lengo likiwa kuiboresha ili ilete tija.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo jana wakati alipotembelea
uwanja huo kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali.
Profesa Mbarawa alisema kwa kiasi
kikubwa mikataba iliyopo imegubikwa na utata na kwamba ipo inayoonesha kuwa
watoa huduma huo wanalipa kwa mwezi, tofauti na makubaliano kuwa malipo
yafanyike kila mwaka.
“Hapa inaonekana watoa huduma wanalipa
kila mwezi, wakati makubaliano ni kila mwaka jambo ambalo ni changamoto, hivyo
iangaliwe ili tuibadilishe. Wiki ijayo nitaunda timu ya wataalamu kwa ajili ya
kupitia mikataba hiyo minne na mingine yote inayohusu uwanja huu,”alisema.
Alisema waliotayarisha mikataba hiyo kwa
kiasi kikubwa hawakuangalia itanufaisha vipi Taifa, hivyo kupitiwa upya
kutasaidia Serikali na wafanyabaishara kupata wanachostahili.
Aliongeza kuwa tangu awali mikataba hiyo
haikuwa mizuri kwa kuwa hakuna kodi zilizokuwa zikikusanywa, hali iliyoikosesha
Serikali mapato.
Kuhusu uongozi, Profesa Mbarawa alisema
ipo haja ya kufanyika maboresho ya uongozi wa uwanja huo na vingine, ili
usimamie vizuri viwanja hivyo kwa kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria badala ya
kusuasua.
“Kama viwanja vya ndege nchini
vikisimamiwa vizuri, vina uwezo wa kukusanya kodi nyingi na maeneo ambayo
awali yalikuwa hayakusanywi kodi, na sasa zinakusanywa yanaonesha mafanikio
makubwa,”alisema.
Alisema kwa kiasi kikubwa uongozi uliopo
sasa ni mzuri, lakini hauendani na kasi anayotaka hivyo kunatakiwa kuwepo watoahuduma
ambao watakuwa wazalendo wa kukusanya kodi.
“Hata kama mtu una matatizo, lazima uwe
mbunifu ili yaishe lakini si kusema kila siku kwamba ni ya kawaida wakati
ukiyaacha yanaendelea kukua jambo ambalo halifai kwa kiongozi,”alisema.
Aliutaka uongozi wa uwanja huo, Idara ya
Uhamiaji na Benki ya NMB kuhakikisha wanakaa pamoja kuangalia namna ya kutatua
changamoto ya utoaji huduma katika eneo hilo, ili wageni wanapoingia nchini
wasitumie muda mrefu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege (TAA), Salim Msangi alifafanua kuwa licha ya kuwepo chagamoto
nyingi kwenye eneo hilo, wamekuwa wakitafuta njia mbadala za kuzipunguza ili
uwanja ulete tija.
0 comments:
Post a Comment