Grace Gurisha
Edward Lowassa |
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameripoti kwa mara
ya tatu Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kama alivyoelekezwa na Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Huo ni mwendelezo mahojiano yake na Polisi baada ya hivi
karibuni kudaiwa kutoa kauli za uchochezi.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema alifikia kwa DCI jana
saa tatu asubuhi akifuatana na baadhi ya wanasheria wa chama hicho, lakini
baada ya mahojiano mafupi alitoka, huku taarifa kutoka ofisi ya DCI ikieleza kuwa
Lowassa anatakiwa kuripoti tena Julai 20.
Lowassa anadaiwa kutoa kauli za uchochezi kwenye futari
iliyoandaliwa Juni 23 na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na baada ya kauli yake
hiyo, alipokea mwito wa DCI ambako alihojiwa kwa saa nne kabla ya kutakiwa
kuripoti tena Juni 29.
Katika futari hiyo, Lowassa anadaiwa kutoa maneno ya
uchochezi kuhusu mashehe wa taasisi ya Uamsho wanaoshikiliwa na magereza, akitaka
utaratibu wa kisheria utumike kuwaachia huru mashehe hao.
Mara ya pili alipofika kwa DCI alitakiwa kurudi tena jana,
huku kauli ya Rais John Magufuli ya kulitaka Jeshi la Polisi kukamata watu wote
wanaozungumzia mashehe hao na kuwahusisha na mauaji yanayoendelea mkoani Pwani,
ikitafsiriwa kuwa huenda hali ingekuwa mbaya zaidi kwa Lowassa.
Hata hivyo, jana hali ilikuwa tofauti huku wakili wake, Peter
Kibatala akisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli alitekeleza agizo hilo kama
alivyoelekeza, kuripoti tena Julai 20, saa 3 asubuhi.
Alisema sababu kubwa waliyoeleza ni kwamba upelelezi
haujakamilika na kubainisha kuwa Lowassa hakukaa kwa muda mrefu kabla ya
kuruhusiwa kuondoka.
“Upelelezi bado haujakamilika ametakiwa kurejea tena Polisi
Julai 20,” alisema Kibatala.
0 comments:
Post a Comment