BRASILIA, Brazil
Luiz Inacio Lula da Silva |
RAIS mstaafu Luiz Inacio Lula da Silva,
amgombea urais anayepewa nafasi kubwa ya kurudi madarakani katika uchaguzi mkuu
wa mwakani, amekutwa na hatia ya rushwa na kuhukumiwa kifungo cha karibu miaka
10 jela.
Uamuzi huo wa Mahakama uliotolewa juzi
ni anguko kubwa kwa Lula, mmoja wa wanasiasa maarufu nchini, na pigo kubwa kwa
fursa ya yeye kutaka kurejea madarakani.
Kiongozi huyo wa zamani, ambaye
alisifika kwa sera zake za kupunguza pengo la utofauti wa kipato nchini,
anakabiliwa bado na mashitaka mengine manne ya rushwa, lakini ataendelea kuwa
huru kutokana na kukata rufaa.
Uamuzi huu unatokana na uchunguzi dhidi
ya tuhuma za rushwa ambao kwa zaidi ya miaka mitatu sasa umeitikisa nchi,
ukijikita katika vitendo hivyo katika ngazi za juu za jumuiya ya
wafanyabiashara na Serikali.
Jaji Sergio Moro alimkuta Lula (71) na
hatia ya kukubali dola milioni 1.2 kama rushwa kutoka kampuni ya uhandisi ya
OAS SA, kiwango cha fedha ambacho waendesha mashitaka, walisema kampuni hiyo
ilikitumia kukarabati hekali lililoko ufukweni kwa ajili ya Lula kama shukurani
ya msaada wake ulioiwezesha kampuni ya Taifa ya mafuta ya Petroleo Brasileiro
(PETR4.SA) kupewa ukandarasi.
Waendesha mashitaka walimtuhumu Lula,
Rais wa kwanza kutoka kundi la wafanyakazi tangu mwaka 2003 hadi 2011, kusimamia
mtandao wa rushwa uliogundulika hivi karibuni kutokana na uchunguzi kuhusu
tuhuma zilizoigubika kampuni ya Petrobras.
Timu ya wanasheria wa Lula ilisema
katika taarifa yake kupitia barua pepe, kwamba hana hatia na itakata rufaa.
“Kwa zaidi ya miaka mitatu, Lula amekuwa
akichunguzwa kisiasa,” waliandika. “Hakuna ushahidi wa maana wa kumweka hatiani
uliotolewa na hata uthibitisho kwamba hana hatia ulipuuzwa.”
Wakili wa Lula, Cristiano Martins amekaririwa
mara kwa mara akimtuhumu Jaji Moro kwa kulalia upande mmoja dhidi ya mteja
wake, tuhuma ambazo Moro anazikanusha.
Moro aliandika kwenye uamuzi wake kwamba
“hakufikia uamuzi huo kama kujifurahisha binafsi, bali ni kinyume chake.
“Inalalamikiwa kwamba Rais wa Jamhuri
amepatikana na hatia ya jinai,” Moro alisema. “Haijalishi una umuhimu gani,
hakuna aliye juu ya sheria.”
Lula atazuiwa kugombea urais iwapo
adhabu yake itaendelea hata baada ya kukata rufaa mahakamani, ambayo
inatarajiwa kuchukua takriban miezi minane hata kutolewa uamuzi.
Asipogombea, mchambuzi wa siasa anasema
Brazili itaingia kwenye msambaratiko na kulazimika kujengwa upya, na pengine
kupata kiongozi ambaye anaweza kujitokeza kwenye kivuli ambacho Lula alikiweka
kwenye siasa za Brazili kwa miongo mitatu.
“Kukosekana kwa Lula kunasababisha uwazi
ndani ya siasa, kunaweka ombwe la madaraka,” alisema Claudio Couto,
mwanasayansi ya siasa wa Wakfu wa Getulio Vargas ambacho ni Chuo Kikuu maarufu.
“Tumeingia katika mvutano mkubwa wa
kisiasa, hata zaidi ya mgogoro tuliokuwa nao mwaka jana.”
Couto alisema anatarajia uamuzi huo
dhidi ya Lula utasimamishwa na Mahakama ya Rufaa. Hali ambayo itafanya mbio za
urais mwakani kuwa wazi na kutoa fursa ya ushindi kwa mwanasiasa kutoka nje, kutokana
na wanaopewa nafasi ya kuwania, nao kuwa wamechafuliwa na tuhuma za rushwa
nchini.
0 comments:
Post a Comment