Mwandishi Wetu
Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu |
JITIHADA za Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kusaidia
uboreshaji huduma za afya hasa kwa wanawake nchini, zimeendelea kuzaa matunda.
Hiyo inatokana na taasisi ya Merck yenye makao yake nchini
Ujerumani kumwahidi kuanzisha mpango wa kugharimia mafunzo maalumu kwa
wataalamu wa afya nchini, hasa ya saratani kwa watoto, matibabu yake kwa
upasuaji na utabibu kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Merck, Dk Rasha Kelej
ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais,
Ikulu, Dar es Salaam, ambako alisema taasisi hiyo imejitolea kuisaidia Serikali
kuboresha sekta ya afya kupitia mpango huo unaotarajiwa kuanzishwa mwishoni mwa
mwaka huu.
Dk Kelej alisema mafunzo hayo kwa wataalamu wa afya
yatatolewa kati ya mwaka mmoja hadi mitatu India, Ulaya na Kenya kwa lengo la
kuboresha upatikanaji huduma zote kuhusu saratani nchini.
Taasisi ya Merck pia ilimhakikishia Makamu wa Rais kuwa itajikita
kuwajengea uwezo wanawake wenye matatizo ya ugumba kwa kuhakikisha wanapata
taarifa sahihi kuhusu matatizo ya ugumba, hivyo itasaidia kubadilisha mtazamo
uliojengeka kwenye jamii kuhusu ugumba kwa wanawake.
Ajenda hiyo itasimamiwa kupitia programu ya Merck More
Than a Mother.
Kwa mujibu wa takwimu za watendaji wa taasisi hiyo,
tatizo la ugumba kwa wanandoa Afrika ni kubwa na inakadiriwa kwamba katika kila
ndoa nne, moja inasumbuliwa na ugumba na karibu asilimia 85 ya ugumba
inasababishwa na ukosefu wa matibabu kwa magonjwa yanayoweza kutibika.
Aidha, Makamu wa Rais aliipongeza taasisi ya Merck kwa
juhudi zake za kuboresha sekta ya afya Afrika na aliikaribisha kufanya kazi
nchini.
Samia alifurahishwa na mipango na mikakati ya taasisi
hiyo na kwamba Serikali iko tayari kushirikiana nayo kuwajengea uwezo kina mama
na utoaji mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya afya nchini hasa kwenye saratani na
ugumba.
0 comments:
Post a Comment