Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Hawra Shamte |
WANACHAMA 764 wa
vikundi vya ujasiriamali vya wilaya nane za Unguja na Pemba, wameshiriki miradi
ya kujiongeza kipato.
Akiwasilisha
jana taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi (WEZA II)
awamu ya pili, Meneja Ushawishi na Utetezi wa Chama cha Wanahabari Wanawake
Tanzania (TAMWA), Hawra Shamte, alisema hatua hiyo imeamsha ari ya kujiendeleza
katika shughuli mbalimbali.
Alisema katika
utekelezaji wa mradi huo, wanawake 7,000 kutoka wilaya hizo walipewa mafunzo ya
kibiashara, usimamizi wa miradi na kupatiwa nyenzo za uzalishaji, jambo lililowawezesha
kupata faida ikilinganishwa na awali katika awamu za kwanza na pili za mradi.
Alisema pamoja
na hatua hizo, pia chama hicho kimewezesha wajasiriamali hao kuunda kamati za
ngazi ya wilaya, ili kukuza na kufuatilia mwenendo wa biashara zao, kusaka
masoko ya bidhaa zao na kujengeana uwezo.
“Kwa lengo la
kuwajengea uwezo na kupanua wigo wa biashara zao, TAMWA Zanzibar iliwapeleka
wajasiriamali wanne kutoka kamati za biashara za wilaya kwenye maenesho ya
kimataifa ya biashara (Sabasaba) yaliyomalizika Dar es Salaam hivi karibuni,” alisema
Hawra.
Aidha, alieleza
kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na taasisi yake bado baadhi ya wazalishaji
wamezoea kuzalisha kizamani kwa kutumia nyenzo duni jambo ambalo linawafanya
kushindwa kuhimili ushindani sokoni.
“Miongoni mwa
wajasiriamali wanaozalisha bidhaa za matumizi ya nyumbani, vyakula, mapambo, walikuwa
wanashindwa kulifikia soko au kuhimili ushindani kutokana na ubora wa bidhaa
zao.
“Hivyo ipo haja
Serikali kuziona juhudi za wajasiriamali hawa na kuwawezesha kupata vifaa bora
vya uzalishaji baada ya sisi kuwapa utaalamu,” alisema Meneja huyo na kuongeza
kuwa baadhi ya bidhaa hizo zina ithibati ya ubora.
Akitoa maelezo
ya utangulizi kuhusu mradi huo, Ofisa Mradi wa TAMWA Zanzibar, Asha Abdi Makame
alisema umelenga kuwajengea uwezo wajasiriamali hao, ili kuendesha na kusimamia
miradi yao na kuongeza thamani ya bidhaa zao.
Wajasiriamali
hao walieleza kuwa mafunzo na uwezeshaji waliopata umewawezesha kuongeza thamani
ya bidhaa zao na kufikia masoko ya nje ya Zanzibar, jambo linaloiwezesha miradi
yao kukua na kupata faida kutokana na uzalishaji.
0 comments:
Post a Comment