Hussein Ndubikile
Angella Kairuki |
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema
Serikali haijatoa tamko kuhusu hatima ya mafao ya watumishi wa umma waliokutwa
na vyeti bandia, huku akibainisha kuwa tamko litatolewa baada ya uhakiki wa vyeti
hivyo kukamilika.
Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam
wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni.
Alisema kuna taarifa za upotoshaji
kwenye mitandao zikieleza kwa namna tofauti jambo hilo hali inayosababisha
sintofahamu miongoni mwa wahusika na kusisitiza kuwa ufafanuzi utatolewa
uhakiki utakapokamilika.
"Hakuna tulikosema watalipwa au
hawatalipwa mafao yao, mwisho wa uhakiki Serikali itatoa ufafanuzi,"
alisema Kairuki.
Waziri Kairuki aliwataka watumishi wa
manispaa kuacha kusambaza taarifa za Serikali, kwani kufanya hivyo ni kwenda
kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.
Aliongeza kuwa changamoto zinazoikabili
Manispaa ya Kinondoni zitafafutiwa ufumbuzi zikiwamo za upungufu wa walimu 50
wa shule za msingi, watumishi 371 wa afya na watumishi wa ardhi na mipango.
Aliwakumbisha maofisa utumishi wa Manispaa
kuwafanyia uhakiki watumishi kabla hawajaingizwa kwenye mfumo malipo ya
mishahara na kwamba Serikali kwenye bajeti ya mwaka 2017/18 kuanzia mwezi huu
hadi Septemba itatoa vibali 52,476 vya ajira mpya.
Alishauri watumishi hao kujikinga na
Ukimwi kwa kubadili nyendo zao na kushiriki kufanya ili kujiepusha na magonjwa
yasiyoambukiza.
Ofisa Utumishi Mkuu wa Manispaa hiyo,
Anna Mwakalyelye alisema hadi sasa mashauri ya nidhamu 134 yanashughulikiwa, 48
yameshashughulikiwa huku 80 yakiendelea kufanyiwa kazi.
Alisema Manispaa imetenga fedha za
kujenga na kuzifanyia ukarabati ofisi za kata za Kinondoni.
Alifafanua kuwa watumishi 372
walipandishwa vyeo na tisa kufanyiwa mabadiliko ya vyeo kulingana na vigezo vyao.
Pia alisema watumishi wanaendelea kupata
mafunzo ili kuwasaidia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Mkuu wa Wilaya, Ali Hapi alimpongeza Waziri
Kairuki kwa utendaji kazi wake na kumwomba atazame kero za upungufu wa
watumishi.
0 comments:
Post a Comment