Mwandishi Wetu, Mwanza
OFISI za Kampuni ya Sahara Media Group (SMG) inayomiliki
kituo cha televisheni cha Star, Radio Free Africa na Kiss Fm zimefungwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa deni la Sh bilioni 4.5, hivyo kuwa
hatarini kupigwa mnada kufidia deni hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusitisha
shughuli za kampuni hiyo kwa kutia kufuli milango yake jana, Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya Udalali ya Sukar, Lyasuka Salehe ambayo ni mawakala wa TRA, alisema
walitoa siku 14 kwa mmiliki wa kampuni hiyo, Anthony Diallo kulipa deni hilo.
"Hizi siku 14 tulizotoa akishindwa kulipa tutaitisha
mnada wa hadhara kukomboa kodi ya Serikali," alisema Salehe.
Meneja wa TRA wa Mkoa wa Mwanza, Ernest Dunde alisema
kazi ya Serikali ni kukusanya kodi, yeyote anayedaiwa lazima alipe hivyo ukusanyaji
madeni ni endelevu na yeyote anayedaiwa lazima alipe.
Meneja wa Utumishi na Utawala wa Kampuni hiyo, Raphael Shilatu alisema ni kweli wamekuwa na
malimbikizo ya kodi ya muda mrefu, huku akitaja sababu kuwa ni Serikali
kuwataka kutoka analojia kwenda dijitali.
"Hali hiyo ilitufanya kuyumba sana kiuchumi baada ya
kufanya uwekezeji mkubwa hivyo kujikuta tumeyumba kiuchumi na kukaribisha
madeni yaliyosababisha hali kama hii," alisema
Shilatu pia aliwataka wapenzi na wasikilizaji wa vyombo
hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu na kuongeza kuwa kipindi hiki ni cha mpito na mambo
yatakuwa sawa.
Kabla ya kufunga milango, wafanyakazi walionekama kupigwa
butwaa huku wengi wao wakitoa magari yao
yasifungiwe ndani.
0 comments:
Post a Comment