Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema hakuna mgonjwa
atakayekwenda kutibiwa kwenye hospitali, vituo vya afya au
zahanati akakosa dawa kwani Serikali imetenga fedha nyingi za kununulia dawa na vifaa tiba.
Majaliwa alisema
hayo juzi, akizungumza na wananchi wa wilaya ya Liwale kwenye mkutano wa
hadhara.
Waziri Mkuu anayefuatana na mkewe, Mary katika ziara ya
kikazi ya siku nne mkoani humo, alisema Serikali haitaki kusikia wananchi wakikosa
dawa.
Alisema moja kati ya ajenda muhimu za Serikali ni
kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ambapo kila mwezi halmashauri zote
nchini zinapelekewa fedha za dawa.
“Serikali ya Rais John Magufuli inatoa fedha za kununulia
dawa kila mwezi katika halmashauri zote nchini. Sasa kama hapa Liwale kuna
malalamiko ya wananchi kukosa dawa, Mkuu wa Wilaya kafuatilie huko Halmashauri
ili kujua wanapeleka wapi fedha za dawa,” alisema.
Katika
Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka
wa fedha 2017/18 Sh bilioni 236 zilitengwa kununulia dawa, vifaa, vifaa tiba na
vitendanishi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema upatikanaji
wa dawa muhimu kwa mwaka 2016/17 iliongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na ya
mwaka 2015/16.
Alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi
Februari Lindi ilipokea Sh milioni 538 za dawa kupitia Bohari Kuu ya Dawa
(MSD).
“Hospitali ya Mkoa ilipokea Sh 195,328,186 za dawa na
ilitumia Sh 127,171,700 kutoka fedha za uchangiaji kununulia dawa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji
wa Halmashauri kwenda vijijini kuelimisha wananchi umuhimu wa utunzaji mazingira ili kuliepusha Taifa na
jangwa.
Pia aliagiza maofisa kilimo kuacha kushinda ofisini na
badala yake waende mashambani kuelimisha wakulima namna bora ya kulima kwa
kufuata njia za kisasa ili kupata tija.
Alitaka kila ofisa kilimo awe na shamba darasa litakalotumika
kuelimisha wananchi.
0 comments:
Post a Comment