Hapi ataka bilioni 5/- zijenge madarasa Dar


Salha Mohamed

Ali Hapi
KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ali Hapi, ametaka wakuu wa vitengo na madiwani kuidhinisha Sh bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Hapi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, amesema fedha hizo ni kwa kila manispaa ikiwa ni pamoja na kuorodhesha matumizi ya kila fedha walizotumia.

Hayo yalibainishwa juzi Dar es Salaam kwenye mkutano uliojumuisha wafanyakazi wa Halmashauri na Manispaa ya Kigamboni kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wilayani Kigamboni.

Hapi alisema tangu Waziri Mkuu akiwa Lindi aagize kila mkoa uhakikishe wanafunzi wote waliofaulu kidato cha kwanza wanapata fursa ya kuendelea na masomo, mkoa huo umekuwa ukichukua hatua mbalimbali ili kufanikisha agizo hilo.

“Nakuhakikishia Waziri Mkuu, Dar es Salaam tumejipanga, tumeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kutuma maombi ya kibali kwa Kamishna wa Elimu ili kuanzishwe zamu mbili za asubuhi na mchana, ili wanafunzi wote wasome kwa wakati mmoja,” alisisitiza.

Alisema miongoni mwa hatua hizo ni ujenzi wa madarasa ambayo fadha zao zinatokana na malipo ya kampuni ya simu ya Zantel ya Sh milioni 687 iliyokuwa ikidaiwa na Halmashauri ya Kinondoni kwa ajili ya kodi ya pango.

Alisema kiasi hicho kitajenga madarasa mengi kwani fedha hizo hazikuwa kwenye bajeti tangu awali kutokana na mikataba yake kunyofolewa na zitatumika kwa ujenzi.

Hapi alikiri kuwa katika Jiji hilo bado kuna changamoto ya upungufu wa madarasa 40 na kutaka wakurugenzi wa manispaa zote za Jiji, kusimamia ujenzi wa madarasa unaoendelea ili hadi Machi 30 uwe umekamilika.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema fedha zitakazotengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ziendane na hadhi ya darasa husika.

Alisema kwa sasa Serikali imeahidi kuongeza kiwango cha ruzuku kwa kila halmashauri huku kila moja ikipaswa kujua matatizo ya halmashauri zao.

Akizungumzia suala la walimu, Majaliwa alisema wamesitisha kuajiri walimu wa masomo ya Sanaa badala yake wanaajiri walimu 4,000 wa masomo ya Sayansi.

"Tayari tumeunda tume ya kupitia mishahara ya watumishi wa umma wakiwamo walimu kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo