Joseph Kulangwa
Joseph Kulangwa |
TANZANIA kama zilivyo nchi zingine
duniani, imekuwa ikipigana vita dhidi ya dawa za kulevya ambazo kwa kiasi
kikubwa zimekuwa zikiathiri vijana na hivyo nguvukazi ya nchi.
Matumizi na biashara ya dawa hizo ni
tatizo lililokithiri maeneo mengi duniani na nchi kadhaa zimekuwa zikitumia gharama
kubwa kwa mapambano hayo, kwa mihadarati ambayo mbali na kufifisha nguvu za
vijana, imekuwa ikikatiza maisha yao.
Athari za matumizi ya dawa hizo ni kubwa
na dhahiri, kwani husababisha watumiaji kuharibikiwa akili na miili na hivyo
kukaa bila kujishughulisha na hata kufanya kazi za kuingiza kipato.
Kuharibikiwa huko kumekuwa kukiwakuta
watumiaji ambao wakati mwingine huwa na kazi nzuri lakini baadaye kujikuta
wakizitelekeza na kuingia katika maisha mapya ya mashaka na hatari zaidi.
Lakini wafanyabiashara ya dawa hizo
wamekuwa wakijinufaisha kwa kujipatia kipato kikubwa na kumiliki mali kubwa
kubwa na za kifahari, huku watumiaji ambao mara zote ni wadogo na masikini,
wakibaki na umasikini wao na hata pengine kupokwa maisha.
Kwa kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya
ni ngumu na ya hatari, ndiyo sababu nchi nyingi hutumia pia gharama kubwa
kupambana huku mataifa kama Mexico, viongozi wakitumia hata mitutu ya bunduki
kukabiliana na wafanyabiashara na watumiaji hao.
Tanzania haijaanza leo kupambana na dawa
za kulevya, ingawa mwaka huu vita hivyo vimeonekana kujitokeza waziwazi hasa kutokana
na njia inayotumika kupambana kwa kutangaza watuhumiwa hadharani na hata wakati
mwingine bila ushahidi wa kutosha.
Kama kuna mtu anapinga vita dhidi ya
dawa za kulevya ni dhahiri haitakii mema nchi hii na watu wake; hivyo kuna haja
ya makusudi ya kuunganisha nguvu Wataznania wote kukabiliana na dawa hizo na
kuzitokomeza ili kubaki na raia wema.
Lakini hata hivyo, kutokana na
maendeleo duniani, kila vita vinahitaji sayansi, kwa maana ya kutafiti, kujiridhisha,
kuthibitisha na kuchukua hatua, badala ya kukurupuka bila utaratibu na hivyo
kukosa ushahidi na uhakika wa mapambano na kuishia kulalamikiwa.
Tanzania ni moja ya nchi ambazo hivi
sasa zinatajwa duniani kuwa si tu vituo, bali hata njia za kupitishia dawa hizo
na matokeo yake vijana wake wengi wamejikuta kwenye uraibu na kuitwa ‘mateja’.
Ili kukabiliana na uraibu huo, baadhi
ya watu waliopata kutumia dawa hizo na kuacha, wameanzisha vituo vya kurekebisha
tabia za watumiaji na kuondoa uraibu, huku Serikali nayo ikisisitiza matumizi
ya dawa za methadone kwa ‘mateja’.
Serikali hivi sasa ina mipango pia, ya
kuhakikisha kwamba inawakusanya ‘mateja’ hao na kuwatafutia maeneo ya kufanya
uzalishaji mali ili kwamba waachane na matumizi ya dawa hizo hatari.
Pamoja na kuanzishwa Mamlaka ya Kuzuia
na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza
na ‘mateja’ na wadau wa kupambana na mihadarati Dar es Salaam, aliahidi
kuwatafutia maeneo ya kuzalishia mali.
Bila shaka hilo ni wazi zuri, lakini linahitaji
nguvu kubwa kuhakikisha na kuthibitisha kwamba ‘mateja’ hao kweli wameachana na
matumizi ya mihadarati na kurudi kwenye hali inayoruhusu uzalishaji mali, ikiwa
ni pamoja na ufundi kwa walio na ujuzi.
Kwa kuwa haina uthibitisho wa asilimia
100 kuwa watumiaji walioacha huacha moja kwa moja kwa kuwa wengine hurudia kama
ilivyopata kutokea kwa Rehema Chalamila ‘Ray C’ na wengine, itakuwa nguvu kwa
watu hao kuaminiwa haraka katika maeneo yao ya ufundi.
Pamoja na nia njema ya Serikali kutaka
kuwasaidia ‘mateja’ hao ambao bila shaka kwa kiasi kikubwa ‘hujitakia’ kuwa na
hali hizo, mimi nadhani mwelekeo ungelenga zaidi watu wenye ulemavu mitaani
walio na elimu lakini hawana cha kufanya.
Sina nia mbaya na ‘mateja’, lakini
kinachofanyika ni kuwalea na kufundisha wengine kwamba kumbe kutumia mihadarati
na kasha kutangaza kuacha, ni njia ya Serikali kumtafutia ‘teja’ eneo la baishara
au uzalishaji mali. Kwa imani hiyo, itakuwa kazi kubwa, ngumu na ya muda mrefu,
kukabiliana na matumizi ya dawa hizo.
Litakuwa jambo la kushangaza sana,
kwamba wakati wenye ulemavu wengi tena wenye ujuzi na sifa za kuajiriwa au hata
kukopeshwa, wamekuwa wakinyanyapaliwa na kuachwa wakitaabika, huku ‘mateja’
wakipewa kipaumbele.
Rais John Magufuli bila shaka kwa
kutambua umuhimu lakini pia usawa wa kibinadamu kwa watu wenye ulemavu, katika
uongozi wake aliamua kuwapa nafasi katika ngazi za juu zikiwamo za naibu
uwaziri na ukatibu mkuu.
Bila shaka alibaini kwamba mchango wao
ni mkubwa, kwa kuamini kuwa ulemavu wa viungo si wa akili, lakini mateja
‘walioguswa’ akili hatuwezi katu kuwalinganisha na wenye ulemavu wa viungo.
0 comments:
Post a Comment