RAIS John Magufuli
ameonekana kuteswa na kusikitishwa na kitendo cha
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kumnyima mkono Rais wa Zanzibar,
Dk Ali Mohamed Shein alipomsalimia wakati wa maziko ya Rais wa Awamu ya Pili
Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi.
Masikitiko hayo aliyatoa jana wakati akihutubia kwenye mkutano wa
hadhara wa kushukuru wananchi wa Zanzibar kwa kumchagua kuwa Rais wa Tanzania,
katika viwanja vya Demokrasia Unguja, ambako alitumia muda mrefu kufafanua
kuhusu mkono huo kwa kauli tofauti tofauti.
Alisema Dk Shein kwa upendo na moyo wake wa huruma, aliamua kumpa
mkono mtu fulani (Maalim Seif), lakini cha kushangaza alikataa kupokea mkono
na kibaya zaidi ilikuwa msibani.
“Juzi wote tumeshuhudia msibani na Watanzania wameona kwenye picha,
Dk Shein kwa unyenyekevu alimsalimu mtu fulani, lakini akakataa. Mkono huo huo
ambao ameukataa, ndio Rais Shein anautumia kusaini fedha za safari na matibabu.
“Kweli una moyo wa upendo, natamani ningekuwa na hata robo maana
mimi nisingeweza kutumia mkono wangu kumsainia mtu akatibiwe, wakati mkono huo
huo aliukataa,” alisema Dk.Magufuli.
Dk Magufuli alisema pamoja na mambo mengine, bado anampongeza
Rais Shein kwa upole, ukarimu na uungwana kwani licha ya kupata asilimia 92 ya
kura zote, ameingiza wapinzani kwenye serikali yake.
‘Hataki’ wapinzani
Alisema yeye hawezi kumuingiza mpinzani kwenye Serikali yake kama
alivyofanya Dk Shein na kufafanua kuwa ndani ya Serikali yake, hatakuwa tayari
kumuingiza mpinzani afanye naye kazi.
“Rais Shein muombe Mungu akupe hata robo ya mawazo yangu.
Natamani niwe na moyo wa aina yako lakini siwezi maana kama mimi ningekuwa nimekataliwa
mkono, tena msibani, nisingesaini hata kidogo fedha kwa ajili ya huyo mtu.
“Jana (juzi) nikiwa Pemba nilikuomba uongeze ukali hata kidogo.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 uchaguzi umekwisha na hautarudiwa
tena ila uchaguzi mwingine ni mwaka 2020. Kwa sasa ni muda wa kufanya kazi
tu,” alisisitiza Dk. Magufuli.
Alisema anafahamu kuwa Zanzibar kuna tatizo la maji lakini tayari
kuna fedha Sh bilioni 200 zimetengwa kwa ajili hiyo, ambapo alirudia kuwa hata
kama kuna watu wanamnyima mikono, aendelee na jukumu la kuhakikisha wananchi
wanapata maji.
Magufuli alisema lazima watu watambue walikotoka, walipo na wanakokwenda
kwa kuwa sasa Zanzibar ni tofauti na ile ya zamani.
Alikumbusha alipokuwa Waziri wa Ujenzi, kwamba alisimamia
upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na anakumbuka hiyo ilikuwa ni kwenye
utawala wa Awamu ya Tatu chini ya mzee Benjamin Mkapa.
Alielezea kushangaa kuona mtu anatoka Zanzibar na kwenda
kuwaambia wageni wasije Zanzibar, lakini cha kufurahisha wamempuuza na wageni
wameendelea kuja maana kuna usemi unaosema kuwa mgeni njoo mwenyeji apone.
*Kufuga ndevu
Magufuli alisema katika maisha yake hakuwahi kufikiria kuwa Rais,
maana alitambua kuwa vyeo vinaletwa na Mungu na kama Mungu amesema hapana ni
hapana tu, hata kama unafuga ndevu namna gani kama Mungu amekataa huwezi kuwa
Rais.
“Rais Shein ana moyo wa upendo kwa watu wote lazima aachwe afanye
kazi yake maana Wazanzibari wameamua ndio awe Rais,” alisema na kuongeza kuwa
wakati Rais Shein anafanya mambo yote kwa ajili ya Zanzibar, anatokea mtu
anamnyima mkono mbele ya waombolezaji waliopo msibani.
Alifafanua kuwa hakuna kitabu chochote au dini yoyote duniani
kinachofundisha chuki badala yake pale watu wanapokoseana, basi wasameheane.
“Lakini hata kwenye msiba uuuwiii,” alisisitiza Rais Magufuli na
kuongeza anatamani kuona nchi inakuwa ya viwanda ili watu wengi wapate ajira
kwani hakuna mtu anayekula chama cha siasa.
Aliomba wananchi wa Zanzibar wadumishe umoja na mshikamano na
kuweka chuki pembeni, kwani ni jambo baya kuona kuna watu wanafanya kazi ya
kufarakanisha watu.
“Mnamkuta mtu na dada yake mmoja CUF na mwingine CCM wewe
unamfarakanisha. Unakuta mtu na mkewe mmoja CUF na mwingine CCM unawafarakanisha
mpaka wanashindwa kulala chumba kimoja, huu ni sawa na ushetani,” alisema.
*Fyoko fyoko
Wakati huohuo Rais Magufuli ameonya kuwa katika utawala wake,
amani ataipa kipaumbele na yeyote atakayeleta fyokofyoko itamrudia mwenyewe.
Alisema msimamo wake hautabadilika na anayetaka kuvuruga amani
atamshughulikia kwani hatamuachia iwe mchana au usiku, iwe asubuhi au jioni na
hata akiwa kitandani, atakayejaribu kuleta chokochoko lazima atamshughulikia.
Magufuli alisema amekwenda Zanzibar kwa dhamira ya kuwaeleza wazi
kuwa katika urais wake, amani itakuwa kitu cha kwanza ndio maana aliwahi kusema
Dar es Salaam atakayeleta fyoko fyoko, atakiona cha mtema kuni.
Alisisitiza kuwa msimamo wake wa pili ni kudumisha Muungano uliopo
kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuulinda kwa nguvu zake zote.
Kipaumbele chake cha tatu, alisema ni kuleta maendeleo ya wananchi
wote bila kujali vyama vyao. “Iwe CCM, iwe CUF, iwe Chadema na hata wasio na
vyama wote nitahakikisha naleta maendeleo yao,” alisema.
*Dk Shein
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli, Dk Shein
alisema vyama vya upinzani vitaiona Serikali ya Zanzibar kama ilivyo, kwa kuwa
kwa kutumia utaratibu wa kidemokrasia CCM hawang’ooki kwani kila uchaguzi
watashinda na kuwagaragaza.
“Baada ya uchaguzi zikatoka kauli kwamba utarudiwa tena, masikini
roho zao, nami huwa nawauliza utarudiwa kwa Katiba gani, na kwa sheria gani?
Maana chini ya Tume ya Uchaguzi ya Mwenyekiti Salimu Jecha, uchaguzi
umemalizika.
“Sheria na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio iliyotoa mamlaka
kwa Tume ya Uchaguzi kuendesha uchaguzi wa rais, wabunge, madiwani na
wawakilishi. Ni katiba ya Zanzibar hakuna katiba nyingine duniani inayoweza
kuitisha uchaguzi tena, hizi ni hadithi ziacheni mitaani, ukweli tutakutana
mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Alisema hakutakuwa na Serikali ya mpito Zanzibar na wanaosema
hivyo wanajidanganya kwani hakuna sababu ya kuwa na serikali ya aina hiyo, kwa
sababu Serikali imeshakuwa madarakani.
*Mafuta na gesi
Kuhusu mafuta na gesi Zanzibar, alisema limepatiwa ufumbuzi wa
kudumu kwa kushirikiana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo walitunga Sheria
ya Mafuta na Gesi na kwa sheria hiyo, Zanzibar ilipewa mamlaka ya kutunga
sheria yake ya mafuta na gesi na imeshapelekwa kwenye Baraza la Wawakilishi
na kikao kijacho cha Septemba 26, itasomwa tena.
“Baraza wakiipitisha wataileta kwangu, nitasaini na kuwa sheria na
kuanza kutumika, baada ya hapo tutaanza kuita wawekezaji na Zanzibar itaanza
kupiga hatua kwa kuwa tuna mambo mazuri ya mafuta na gesi,” alisema.
Alisema atashirikiana na Rais Magufuli kutekeleza sheria hiyo,
pamoja na kuiwezesha Zanzibar kukuwa kiviwanda hasa vya samaki.
Aliongeza kuwa Zanzibar imeendelea kukusanya kodi ipasavyo, kwani
hivi sasa mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Alitoa mfano wa 2011
walipokuwa wakikusanya Sh bilioni 13 kwa mwezi, wakati sasa wanakusanya Sh
bilioni 52.
“Pesa hazitutoshi lakini tunazo, tumewalipa wastaafu takribani Sh
bilioni 16, tunatoa mishahara kwa wakati na utalii umetuingizia fedha za kigeni
kwa zaidi ya asilimia 80,” alisema.
0 comments:
Post a Comment