Fidelis Butahe, dodoma
WABUNGE vijana wameishauri
Serikali kubadili mfumo wa elimu wakieleza kuwa umekuwa chanzo cha vijana wengi
nchini kushindwa kujiajiri na kutegemea kuajiriwa.
Wakizungumza katika semina kwa
wabunge vijana iliyofanyika jana mjini Dodoma, wabunge hao walisema hata wale
wanaosaka ajira, hukwama kwa kigezo cha uzoefu huku baadhi wakihoji sababu za
wanafunzi waliofeli kutowekewa utaratibu wa kuendelea na masomo.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema),
Lucy Mollel alisema: “Mfumo wa usimamizi wetu wa elimu umekuwa janga, hatujui
tunataka kuzalisha kundi lipi la vijana.”
Aliongeza: “Miaka ya nyuma
kulikuwa na utaratibu wa watu walioshindwa Kidato cha Sita kufanya mitihani
fulani na kuendelea na masomo ila kwa sasa hakuna. Juzi tumeshuhudia jinsi
wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma walivyofukuzwa badala ya kusaidiwa. Uamuzi ule
wa Rais Magufuli (John) umewanyima fursa ya kuweza kujikwamua.”
Alisema Serikali haipo kwa ajili ya
kuwahukumu vijana na kwamba wanafunzi kufukuzwa kwa kigezo cha ufaulu mdogo, si
jambo la busara.
Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid
Shangazi alisema ni muhimu kwa Serikali kuboresha Sera ya Elimu ili iendane na
mazingira ya sasa na kuwaandaa vijana vizuri.
“Ili tuweze kufanya jambo lazima
tuboreshe sera ya elimu ili imuandae kijana awe na fikra za ujasiliamali na
kujipatia kipato,” alisema Shangazi.
Mbunge wa Serengeti (Chadema),
Marwa Chacha alisema elimu ni tatizo kubwa kwa vijana kwa maelezo kuwa ni ngumu
kumkuta kijana aliyemaliza chuo amejiajiri na kutoa mfano jinsi miaka ya nyuma
wanafunzi walivyokuwa wakifundishwa elimu ya kujitegemea, jambo alilosema kwa
sasa halipo.
“Kama vijana lazima tuhakikishe
kuwa mfumo wetu wa elimu unabadilika na hili tuliseme bungeni, lazima tuhoji
hawa wanafunzi wanaofeli na kushindwa kuendelea na masomo wanasaidiwa vipi?”
alihoji.
0 comments:
Post a Comment