WATU 13 wamepoteza maisha na wengine 11 kujeruhiwa kwenye ajali ya magari mawili yaliyogongana kwenye makutano ya barabara kuu za Mwanza-Shinyanga na ya kutoka kijiji cha Mwamaya wilayani hapa.
Ajali hiyo
ilitokea jana saa 12:15 asubuhi ikihusisha basi dogo aina ya Toyota Hiace na
basi kubwa la abiria lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Mwanza.
Akizungumza
jana kwa simu kuhusu ajali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed
Msangi alisema Toyota Hiace ikitoka Mwamaya ikiendeshwa na Kurwa John,
iligongana na basi la Super Shem.
Msangi
alisema katika ajali hiyo watu 10 walipoteza maisha papo hapo wakiwamo watoto
wawili, ambapo majeruhi watatu walifariki dunia wakiwa njiani na kwenye
hospitali ya Ngudu wilayani Kwimba ambako walipelekwa kutibiwa majeraha
waliyopata.
Kamanda
alisema kwenye ajali hiyo watu 11 walijeruhiwa na kukimbizwa kwenye hospitali
hiyo ya wilaya lakini 10 kutokana na hali zao kuwa mbaya walihamishiwa kwenye Hospitali
ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC).
Alidai kuwa
chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Hiace ambaye alikuwa kwenye mwendo kasi na
bila kuchukua hadhari aliingia kwenye barabara kuu na kukumbana na basi hilo
lililokuwa likiendeshwa na Kisoka Shirima.
“Hili basi
la Super Shem lilikuwa likitoka Mbeya kuja Mwanza lakini usiku lilipumzika
Shinyanga na liliondoka asubuhi kufika Mwamaya kwenye makutano na barabara kuu ya
Mwanza-Shinyanga likakutana na Hiace ambayo dereva wake aliingiza bila hadhari
likagongwa na kusababisha watu 10 kupoteza maisha papo hapo na majeruhi,”
alisema Kamanda Msangi.
Alieleza
kuwa dereva wa Hiace, anadaiwa kutoroka baada ya ajali hiyo huku wa Super Shem
akijeruhiwa pekee yake kati ya waliokuwa kwenye basi hilo.
Alisema
dereva huyo alibanwa na usukani lakini bado polisi wanawachunguza majeruhi
waliopo hospitali ili kumbaini dereva anayedaiwa kutoroka kama ni miongoni
mwao.
Kamanda
Msangi alisema baadhi ya miili ya marehemu hao ambao wengi ni wa kijiji cha
Mwamaya imetambuliwa na majeruhi mwingine anadaiwa alipelekwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Misungwi.
Hii ni ajali
ya pili mbaya kutokea ndani ya siku mbili baada ya ile ya usiku wa kuamkia juzi
mkoani Njombe iliyotokana na kupinduka kwa basi la kampuni ya New Force na
kusababisha vifo vya watu 12 na wengine 28 kujeruhiwa.
0 comments:
Post a Comment