WAKATI Rais John Magufuli akiahirisha safari ya Zambia ili kushughulikia athari za tetemeko la ardhi Kagera, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesitisha shughuli zake na kwenda mkoani humo kupata taarifa za kina juu ya athari zilizotokea.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari
jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene,
Mwenyekiti huyo pia atatembelea maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo pamoja na sekondari
ya Ihungo ambayo Mwenyekiti huyo alisoma kidato cha tano na sita.
“Kutokana na madhara makubwa, vikiwamo vifo, majeraha na
uharibifu wa makazi uliosababishwa na tetemeko la ardhi Jumamosi, Mwenyekiti wa
Chama Taifa amelazimika kukatisha ratiba ya shughuli za kikazi na yuko safarini
kwenda Kagera,” alisema.
Makene alisema Mbowe akiongozana na viongozi wa Chadema
na Serikali, waatanzia ziara mjini Bukoba na baada ya kupata taarifa ya kina
juu ya athari zilizopo hadi sasa, atapita maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo.
Alisema mojawapo ya maeneo ambayo Mwenyekiti atakwenda
kujionea athari kubwa zilizotokea ni pamoja na sekondari Ihungo ambayo
Mwenyekiti huyo alisoma, ambapo inaelezwa kuwa shule hiyo ni moja ya maeneo
yaliyoathiriwa sana na janga hilo.
“Mwenyekiti atafika kuwapa pole na kuwafariji waathirika wa
tetemeko, waliofiwa, waliojeruhiwa na ambao walilazimika kujihifadhi kwenye
viwanja vya mpira baada ya makazi yao kuharibiwa,”alisema Makene kupitia
taarifa hiyo.
Aliongeza kuwa chama hicho kinaendelea kutoa pole kwa
waathirika wa tetemeko hilohuku kikitoa mwito kwa Watanzania kuendelea kuguswa
na kuwa pamoja na waliokumbwa na maafa hayo.
0 comments:
Post a Comment