Peter Kimaro
KADIRI siku zinavyozidi kwenda, ndivyo teknolojia inazidi kukua na kuja na mambo mapya. Kwa sasa Kampuni Simu Tanzania (TTCL), wameleta teknolojia mpya ya TTCL TV ili kuboresha na kurahisisha mchakato mzima wa upashanaji habari.
Teknolojia hii inamuwezesha mtumiaji wa simu ya mkononi kutazama televisheni kupitia simu yake.
Mtaalamu wa Bidhaa za Mawasiliano wa TTCL, John Yahaya anasema teknolojia inayomuwezesha mtu kutazama televisheni kupitia simu yake ni Internet Protocol Television (IPTV).
“TTCL tumetumia teknolojia hiyo kuwaletea huduma hii, na ili kuipata unatakiwa kuwa na simu kadi ya TTCL ambayo sisi tutakuunganisha moja kwa moja kwenye huduma,” anasema.
Yahaya anasema teknolojia hiyo haichagui aina ya simu ilimradi simu kadi ya TTCL imesoma katika simu ya mteja, na hapo anaweza kupata huduma hiyo, ila simu zisizo na uwezo wa kupokea intaneti hazihusiki na huduma hiyo.
“Simu ambazo zinahusika zaidi kwenye huduma hii ni smart phone kwa kuwa zina kioo kikubwa ambacho kinamuwezesha mtumiaji kuona picha kubwa na yenye ubora zaidi.
“Tunapendekeza smart phones kwa sababu mtumiaji anapaswa kupakua (download) programu kwenye mtandao (play store au google play) itwayo TTCL TV player, kisha ahifadhi kwenye simu yake ili kumuwezesha kupata huduma hii.
“Kupakuwa programu ni bure kinachotakiwa ni simu iwe imeunganishwa na intaneti, kisha utajiunga na vifurushi vya TTCL TV ambayo ni tofauti na vifurushi vya intaneti,” anasema.
Anasema kuna vifurushi vya siku, wiki, na mwezi na ikiwa mteja atajiunga na kifurushi kimojawapo ataangalia televisheni bila kikomo hadi pale muda wa kifurushi husika utakapoisha.
Yahaya anasema kwa sasa huduma hiyo ina chaneli zaidi ya nane za hapa nchini na nje na kwamba hivi karibuni wanatarajia kuongeza chaneli zaidi ya 16 ambazo zitakuwepo na za michezo.
Mtaalamu huyo anasema kuwa wameingia ubia na kampuni ambayo imesajiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo kazi yake ni kukusanya maudhui kutoka chaneli mbalimbali, na waliridhia TTCL kutoa hiyo huduma kupitia simu za mkononi.
Anasema huduma hiyo si kwa watumiaji tu wa si za mkononi, bali hata kwa watumiaji wa majumbani ambao wameunganishwa na TTCL.
“Mteja wa nyumbani anahitajika kuwa na simu kadi na kifaa kiitwacho Set top box ambacho kinafanya kazi kama king’amuzi, na mteja atakuwa na uwezo wa kuangalia televisheni,” anasema.
Faida zake
Anasema kuna baadhi ya maeneo huwezi kutembea na televisheni, lakini simu ya mkononi unaweza kutembea nayo sehemu yoyote, hivyo huduma itamuwezesha mtu kujua nini kinaendelea katika televisheni.
“Uzuri ni kwamba kipindi vyote haviwi vimerekodiwa bali vinakuwa ni vya moja kwa moja (laivu).
“Pili wamiliki wa televisheni wataongeza watazamaji (viewership base) kitu ambacho wenyewe wamekuwa wakikililia kwa muda ili waweze kufanya biashara,” anasema.
Meneja usambazaji wa TTCL, Rober Noel anasema kabla mwaka huu kumalizika watakuwa wameshapeleka huduma hii katika mikoa zaidi ya 12 ya Tanzania.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment