WABUNGE wa vyama vinavyounda Ukawa jana walipinga kitendo chaNaibu Spika, Dk Tulia Ackson, kuwazuia kusoma utangulizi wa maoni ya wapinzani kuhusu miswada miwili iliyowasilishwa bungeni, kwa maelezo kuwa yana maneno yanayoiponda Serikali kuzuia vyama vya upinzani kufanya shughuli za siasa.
“Tuendelee ila nawaomba mkatizame filamu inaitwa The Great
Dictator. Nadhani ujumbe umefika,” alisema Mbunge wa Tarime Mjini, Esther
Matiko (Chadema) wakati akisoma maoni ya upinzani ya Wizara ya Afya, Maendelepo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa niaba ya msemaji wa upinzani wa wizara
hiyo, Mbunge wa Siha, Godwin Mollel (Chadema).
Mbali na Matiko aliyesoma maoni ya Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji
wa Baraza la Wanataaluma wa Kemia, hata Mollel aliyesoma maoni ya Muswada wa
Sheria ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, naye
aliwataka wahusika kupokea ujumbe huo, hata kama umezuiwa kusoma.
Mara zote ambazo walianza kusoma utangulizi wa maoni hayo, Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Dk Abdallah Posi alisimama na
kuomba mwongozo kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk Ackson kwamba kinachozungumzwa na
wasemaji hao, hakiendani na maana ya miswada hiyo.
Tangu kuanza kwa vikao vya Bunge Jumanne iliyopita, jana ndio ilikuwa
siku ya kwanza kwa Dk Tulia kuongoza kikao cha chombo hicho cha kutunga sheria,
hivyo mvutano huo kutafsiriwa kama mwendelezo wa vita kati ya wapinzani na
Naibu Spika huyo.
Katika mkutano wa Bunge wa Bajeti lililohitimishwa Juni 30, wabunge
wa Ukawa, inayoundwa na vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, NLD na CUF walikuwa
wakitoka ukumbini kila wakati Dk Tulia alipoongoza vikao, wakidai kuwa hawana
imani naye kwa kuwa anawabagua na kukandamiza demokrasia ndani ya chombo hicho.
Hata hivyo, uamuzi wa Spika wa Bunge Job Ndugai na viongozi wa dini
kuonyesha utayari wa kushughulikia madai hayo, uliwarejesha wabunge hao bungeni
na kumaliza siku 32 za kususia vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia.
0 comments:
Post a Comment