Jaji Damian Lubuva |
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa NEC,
Jaji Damian Lubuva, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa Tume
za Uchaguzi za Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
uliomalizika hivi karibuni Botswana.
Jaji Lubuva alisema katika mkutano huo ambao alifuatana
na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
walijifunza mambo mengi ambayo wanaweza kuyatumia kwenye uchaguzi ujao
kulingana na sheria za nchi likiwamo suala la kutumia vitambulisho hivyo na
kuachana na vya mpiga kura.
“Katika mkutano ule tulijifunza mengi ambayo tungeweza
kuyatumia kuboresha uchaguzi wetu lakini kwa sasa ambalo naweza kusema
tuliangalie ni kutumia kitambulisho cha Taifa kama kadi ya mpiga kura lakini
hili litatarajia pia na sheria zetu,’’ alisema Jaji Lubuva.
Alisema katika nchi zinazotumia vitambulisho hivyo,
sheria zao zinawataka kufanya hivyo tofauti na nchini ambapo sheria inataka kutumia
kadi ya mpiga kura.
Alisema katika uchaguzi ujao endapo Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (Nida) itakuwa imekamilisha kuandikisha wananchi wote na
kuwapa vitambulisho, NEC itaangalia sheria ilivyo na kushauri namna ya
kuifanyia marekebisho.
“Kuna baadhi ya mambo ambayo tuliona kwa wenzetu ambayo
yanafaa kuigwa na ni mazuri, kwa mfano hilo la kutumia kitambulisho cha Taifa,”
Jaji Lubuva alisema.
Suala lingine lilihusu kuruhusu Watanzania walio nje ya
nchi ambapo alisema ili kulifanyia uamuzi mzuri ni vema likapelekwa taratibu na
kuangalia faida na athari zake.
Alisema katika mkutano huo baadhi ya wajumbe wa tume za
nchi wanachama ambao walikuja nchini kuona uchaguzi wa Oktoba mwaka jana,
walipongeza namna uchaguzi huo ulivyofanyika kwa uhuru na uwazi na pamoja na
ushindani mkubwa, ulimalizika salama.
“Moja ya mambo ambayo wenzetu pia walijifunza kwetu ni
jinsi tulivyoandikisha idadi kubwa kwa miezi michache, huku kukiwa hakuna vifaa
vya kutosha na jinsi uchaguzi wetu ulivyokuwa na ushindani lakini tukatoka
salama,’’ alisema.
0 comments:
Post a Comment