Mwandishi Maalumu, New York
Dk Augustine Mahiga |
TANZANIA
imezitaka nchi zilizoendelea kuwajibisha wawekezaji na kampuni zao ili walipe
kodi.
Hayo
yalielezwa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dk Augustine Mahiga wakati akihutubia Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa (UN)
na kutumia fursa hiyo kuelezea vipaumbele vya Serikali ya Tanzania.
Waziri
Mahiga alifafanua kuwa, lengo namba 16 la maendeleo endelevu linatambua kuwa
rushwa inakandamiza juhudi za kupambana na umasikini na kuleta usawa wa jinsia,
kwani inazuia fursa.
Katika
muktadha huo, alisema serikali ya Tanzania imeanzisha vita dhidi ya rushwa kwa
kuhuisha uwazi, uwajibikaji na usahihi katika utoaji huduma kwenye taasisi
zake.
Alisisitiza
kwamba Serikali imeweka misingi mizuri ya uwajibikaji inayomtaka mtumishi wa
umma kutambua kwamba wajibu wa kwanza ni kutoa huduma bora na kwa wakati kwa
umma.
“Juhudi
hizi za Serikali za kupambana na rushwa hazitazaa matunda bila kuungwa mkono na
jumuiya ya kimataifa. Nchi zilizoendelea zinatakiwa kuwajibisha wawekezaji wao
pamoja na kampuni zao ili kulipa kodi stahiki,” alieleza zaidi Waziri Mahiga.
Aliongeza:
“Ni lazima wawe tayari kurudisha mali na fedha zilizoibwa kutoka nchi zinazoendelea
na kuzificha katika nchi zao ili mali na fedha hizo zisaidie maendeleo yetu.”
Kuhusu fursa
za jinsia na uwezeshwaji wanawake, Waziri Mahiga alielezea juhudi ambazo
zimefanywa na Serikali katika kuwezesha wanawake ikiwamo kushika ngazi za juu
za uamuzi kuanzia Serikali Kuu hadi Bunge na uwezeshwaji kiuchumi.
Katika
kuthibitisha kuwa Tanzania inazingatia usawa wa jinsia katika uteuzi wa ngazi
za uamuzi, Waziri Mahiga alieleza kwamba, kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi
mkuu wa mwaka jana, Rais John Magufuli aliteua mwanamke kuwa Makamu wa Rais.
“Uteuzi huu
unathibitisha nia ya nchi yangu ya kuona wanawake wengi zaidi wanakuwa kwenye
nafasi za juu za uamuzi. Na ajenda hii ya uwezeshaji wanawake sasa inamilikiwa
na wanawake wenyewe,” alisisitiza Waziri. Kwa vijana, kiongozi huyo wa ujumbe
wa Tanzania aliyemwakilisha Rais wa Tanzania, alisema.
Vijana ni
nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote, si tu kwamba ni viongozi wa kesho lakini
pia wa sasa.
Alihadharisha
kwamba kutowapa kiupaumbele vijana ni kujitafutia matatizo makubwa kutokana na
alichosema ni rahisi kurubuniwa na makundi hatari kwa ustawi wa jamii na Taifa.
“Kutoka na
kwamba idadi ya vijana ni kubwa, Serikali inachukua hatua mbalimbali za
kuwezesha kundi hili la jamii ambalo ni muhimu katika utekelezaji wa ajenda
2030. “Na ili vijana watekeleze jukumu hilo, Serikali imeanzisha mfuko wa
maendeleo wa vijana ambao hadi Machi jumla ya Sh bilioni 1.6 zilipelekwa kwa
vikundi 284 vya vijana,” alisema.
Kuhusu
elimu, eneo ambalo ni kipaumbele kingine cha Tanzania, Waziri alieleza kuwa upatikanaji
elimu jumuishi na ya viwango, ndicho kipaumbele cha Serikali kwa kuwa inaamini
kuwa, elimu ni ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu.
Alifafanua,
kuwa Serikali inahakikisha kwamba watoto wote wanapata elimu bure kuanzia shule
ya msingi hadi sekondari. Pamoja na kutoa elimu bure, imeboresha mitaala yake
kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.
“Alipoingia
madarakani, Rais Magufuli alitangaza kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari
kuwa bure. Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 263 ili kuhakikisha elimu
inakuwa bure kwa wote.
Vipaumbele
vingine vya Tanzania ambavyo Waziri aliviainisha ni pamoja na mikakati ya
Serikali imejiwekea katika utekelezaji wa mkataba wa mabadiliano ya tabia nchi
utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, mapambano dhidi ya dawa za
kulevya na kukabiliana na ugaidi ambao alisema ni tatizo ambalo linaendelea
kukua na kuwa tishio hata kwa Afrika Mashariki.
0 comments:
Post a Comment