Fidelis Butahe
KUFA kufaana.
Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantius Msole
na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda kutumia
maafa ya tetemeko la ardhi mkoani humo kujinufaisha binafsi.
Badala ya
misaada kufikia wananchi wanaosota, huku baadhi wakikosa mahala pa kuishi
imefikia mikononi mwa viongozi hao wawili.
Wateule hao
wa Rais John Magufuli ambao hivi karibuni walikula kiapo cha uadilifu wa
utumishi wa umma katika hafla iliyofanyika Ikulu, wamebainika kufungua akaunti
zingine za benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa
iitwayo ‘Kamati Maafa Kagera’, kwa lengo la kujipatia fedha.
Hata hivyo,
ulaji huo waliojitengenezea umewatokea puani, baada ya Rais kutengua uteuzi wao
na kuviagiza vyombo vya Dola kuwachukulia hatua za wote waliohusika katika
njama za kufungua akaunti hiyo.
Kama hiyo
haitoshi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa
huo, Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika na njama hizo.
Akaunti
hiyo ya maafa ilifunguliwa kuwezesha watu wa kada mbalimbali kuchangia maelfu
ya wananchi waliokosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264
kupata nyufa yakiwamo majengo 44 ya taasisi za umma. Tetemeko hilo lilitokea
Septemba 10 na kusababisha vifo vya watu 17.
Uamuzi wa
Rais ulitolewa jana na Majaliwa muda mfupi baada ya kupokea hundi ya msaada wa Sh
milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ambayo iliwasilishwa
kwa niaba yake na balozi wa nchi hiyo nchini, Sandeep Arya kwa ajili ya
waliokumbwa na maafa hayo.
“Natoa
mwito kwa wananchi na taasisi kuendelea kuchangia misaada kwa walioathirika kwa
kutumia akaunti rasmi ya ‘Kamati Maafa Kagera’, ambayo imetangazwa na Serikali,”
alisema Majaliwa.
Taarifa
iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, haikuweka wazi
kiasi ambacho wateule hao wa Rais walichota kupitia akaunti hiyo bandia, wala
muda walioifungua, baada ya Serikali kutangaza akaunti yake rasmi.
Sakata hilo
liliibuka huku baadhi ya wananchi wa Bukoba wakisota na kulalamika kukosa
baadhi ya mahitaji muhimu huku Serikali ikihaha kusaka misaada kila kona kwa
kupokea michango kutoka kwa mashirika, taasisi, viongozi na watu mbalimbali.
Awali,
katika makabidhiano ya hundi hiyo, Arya alisema Waziri Mkuu wa India alisema
Serikali na wananchi wa nchi hiyo walipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za
kutokea kwa maafa hayo yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.
Rais
Magufuli alimshukuru Waziri Mkuu huyo na Serikali yake kwa kutoa mchango huo na
kwamba aliguswa na moyo wa upendo walioonesha.
“Balozi
Sandeep Arya naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu,
mwambie kwa niaba ya Serikali yangu tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu
muhimu kwa ajili ya Watanzania wenzetu waliopatwa na maafa Kagera,” alisema Rais.
“Tumefarijika
kwamba marafiki zetu mmeguswa kwa namna ya kipekee na tatizo lililoipata nchi
yetu.”
0 comments:
Post a Comment