BARAZA la Mitihani la Tanzania (Necta), limetangaza
kuanza kwa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE), utakaofanyika leo na
kesho nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam,
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema jumla ya watahiniwa
waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 795,761 tofauti na mwaka jana ambapo
walikuwa 775,729 .
Alisema kati ya wanafunzi hao wavulana ni 372,883 sawa na
asilimia 46.86 na wasichana ni 422,878 sawa na asilimia 53.14 watakaofanya
mitihani kwenye shule 16,350.
“Kati ya watahiniwa wote waliosajiliwa, watahiniwa
765,097 watafanya mitihani yao kwa Kiswahili na wengine 30,664 watatumia
Kiingereza ambacho wamekuwa wakikitumia kujifunzia,’’ alisema Dk Msonde
Alisema watahiniwa wasioona waliosajiliwa kufanya
mitihani ni 95 wakiwamo wavulana 57 na wasichana 38, wenye uono hafifu ambao
huhitaji maandishi makubwa ni 810 kati yao wavulana ni 402 na wasichana ni 408.
Alisema masomo yatakayofanyiwa mitihani ni Kiingereza,
Kiswahili, Hesabu, Sayansi, Maarifa ya Jamii ambapo somo la Tehama
halitafanyiwa mitihani kwa sababu ni shule chache tu zilizokuwa zinafundishwa
bila vifaa vya kutosha.
Alisema maandalizi ya mitihani yamekamilika ikiwa ni pamoja
na kusambazwa kwa karatasi, fomu maalumu za OMR za kujibia na nyaraka zote
muhimu zinazohusu mitihani katika halmashauri zote nchini.
Dk Msonde, alitoa mwito kwa walimu na wanafunzi kuwa
waaminifu kwenye mitihani huku akizitaka jamii zinazozunguka maeneo ya shule
kuwa tulivu katika kipindi ambacho wanafunzi watakuwa wanafanya mitihani yao.
“Tunatoa mwito kwa wasimamizi kufanya kazi yao ya usimamizi
kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu,B araza halitasita kuchukua hatua kwa
mtu atakayehusika na udanganyifu wa mitihani,’’alisema Dk Msonde.
0 comments:
Post a Comment