* Watu binafsi, mashirika, kampuni, balozi wachangia
* Baadhi watoa fedha taslimu, vifaa, saruji, kujenga shule
KUGUSWA na tukio la tetemeko la ardhi lililotokea
Jumamosi mkoani Kagera na uhamasishaji uliofanywa na Serikali, umewezesha
misaada mingi kutolewa kwa waathirika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana kutokana na vyanzo
mbalimbali watu, binafsi, kampuni, mashirika na ofisi mbalimbali zikiwamo
balozi zinazowakilisha nchi zao nchini zimechangia zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Makundi hayo yalikutana jana Ikulu Dar es Salaam katika
mkutano maalumu wa kuchangia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera
ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Wafanyabiashara hao kwa nyakati tofauti walitoa ahadi za
kuisaidia Serikali huku Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi akiwasihi
kwamba kundi hilo ndilo linalopaswa kuchangia kwa wingi kutokana na kuwa ni
nchi yao.
"Tanzania inapaswa kusaidiwa na Watanzania wenyewe
hivyo ni vema kila mmoja kwa nafasi yake asaidie katika hili," aliasa.
Balozi
Ubalozi wa China nchini ulitoa Sh milioni 100 na kupeleka
madaktari, helikopta sita, chakula, mahema na madawati huku wa Japan ukiahidi
kuangalia namna utakavyoweza kuchangia.
Umoja wa Mataifa (UN) uliahidi kusaidia kurejesha miundombinu
mkoani humo.
Wafanyabiashara
Mohamed Dewji kupitia kampuni ya Mohamed Enterprises na
Mo Foundation walitoa Sh milioni 100, Salum Turky, kupitia kampuni ya Muza Oil
Mills aliahidi kutoa saruji mifuko 5,000 na mabati 3,000 huku Mengi akiahidi Sh
milioni 110.
Kampuni ya Toyota ilitoa Sh milioni 10, Subash Patel kupitia
kampuni zake aliahidi Sh milioni 150, Kamal Group Sh milioni 50 na Urban Group
Sh milioni 20 kusaidia ujenzi wa miundombinu.
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) iliahidi Sh milioni 100,
IPTL Sh milioni 50, Azania Group walitoa Sh milioni 20, Tanzania Agricultural
Processing Zone Sh milioni 30 na Tacosoa Sh milioni 250.
Pia Group Six walitoa tani 80 za saruji, Kagera Sugar Sh
milioni 100 na tani 10 za sukari, Jambo Plastics Sh milioni 20, mdau wa Bukoba
Melisa Kataraiya Sh milioni 20.
Kampuni nyingine ni Tanga Cement mifuko 1,000 ya saruji,
Pepsi Sh milioni 50, Kiwanda cha Bia cha Serengeti mifuko 800 ya saruji, JBP,
OIL COM na MOIL watajenga shule mbili zilizoharibika kwa tetemeko hilo.
Pia kampuni ya Puma waliahidi Sh milioni 50, Agusta Tanzania
Sh milioni 10, Kampuni ya Tipper Sh milioni 20 kusaidia ujenzi wa miundo mbinu,
Camel Oil kupitia kampuni ya Camel Cement mifuko 1,000 ya saruji kusaidia
ujenzi wa nyumba zilizoharibika.
Jumuiya ya Waislamu wa Madhehebu ya Imamu Shafi Sh
milioni 100, Sahara Tanzania Sh milioni 20, Engen Petroleum Sh milioni 10.
Awali Majaliwa aliwashukuru wafanyabishara na mabalozi
hao kwamba alikuwa anatafuta nafasi ya kukutana nao kikao cha pamoja, akisema
nafasi hiyo bado ipo na mkutano huo wa jana ulikuwa maalumu kwa ajili ya
kuchangia waathirika wa mafuriko.
Alisema Serikali imefungua akaunti CRDB namba
015225617300 yenye jina la Kamati ya Maafa Kagera, na hivi karibuni
zitatangazwa namba za M Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money kwa wanaoweza kuchangia
kwa njia hiyo.
Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Aziz Mlima, alisema Jumamosi yatafanyika matembezi ya
hisani ya yatakayoanzia Oysterbey Polisi hadi Masaki ili kuchangia Sh milioni
10 kwa ajili hiyo.
Naye Fidelis Butahe, anaripoti kutoka Dodoma kwamba
wabunge wote bila kujali itikadi zao waliridhia kwa kauli moja kukatwa Sh
220,000 ya posho ya kikao cha jana ili kusaidia maafa hayo.
“Posho ya leo ya wabunge itachangia maafa ya wananchi wa
Kagera. Wabunge tusimame kwa dakika moja kama ishara ya kuwakumbuka ndugu zetu
walioathirika na kupoteza maisha katika maafa haya,” alisema Dk Tulia jana.
Wakati Serikali ikitoa taarifa bungeni jana kuhusu maafa
hayo iliyosomwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene
kwa niaba ya Waziri Mkuu, wabunge wa upinzani walisema kilichopaswa kuelezwa si
nyumba na shule ngapi zimebomoka, bali misaada waliyopewa wananchi waliopata
maafa mpaka sasa.
0 comments:
Post a Comment