* Serikali yapania kutangaza nauli nafuu
* Ndege mpya kutua karibu viwanja vyote
* Ndege mpya kutua karibu viwanja vyote
Sharifa
Marira
WATANZANIA wengi wanatarajiwa kuanza kunufaika na usafiri wa anga,
kutokana na unafuu wa huduma hiyo utakaowezeshwa na ndege mpya za Shirika la
Ndege Tanzania (ATCL).
Akizindua jana Dar es Salaam, ndege hizo aina ya Bombardier Q 400,
Rais John Magufuli mbali na kutaja madhambi ya Shirika hilo, alielezea unafuu
wa ndege hizo mpya, unaotarajiwa kuonekana mpaka kwa wateja.
Akitolea mfano wa safari ya kutoka Dar es Slaam kwenda Mwanza, Rais
Magufuli alisema gharama ya mafuta ya kurusha Bombardier Q ni Sh milioni moja
wakati ndege zingine ikiwemo Boeing, gharama ni Sh milioni 28.9.
Kutokana na gharama kubwa ya kurusha ndege zinazotumika katika usafiri
wa anga kwa sasa kabla ya ujio wa Bombardier Q, Rais Magufuli alisema nauli ya
usafiri kati ya Dar es Salaam na Mwanza, ilifikia Sh 800,000.
Alifafanua kuwa kutokana na ujio wa Bombardier Q mbili, moja ya mashirika
yaliyokuwa yakitoa huduma hiyo nchini, limeamua kupunguza wafanyakazi, baada ya
kupata habari ya ujio wa ndege nafuu. Kuhusu kasi ya Bombardier Q, ikilinganishwa
na ndege zingine ambazo zimekuwa zikitoa huduma hiyo nchini, Rais Magufuli huku
akitumia mfano wa Dar es Salaam- Mwanza, alisema tofauti ni dakika 20 tu.
“Dakika 20 ni nini katika unafuu wa usafiri?” Alihoji Rais
Magufuli, huku akisisitiza kuwa ndege hizo hazijaandikwa CCM, hivyo ni za
Watanzania wote na kila mmoja, akiwemo Mbowe (Freeman- Mwenyekiti wa Chadema)
na Lipumba (Profesa Ibrahim-aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF), watapanda.
Ndege hizo ambazo zina uwezo wa kutua katika viwanja ambavyo havina
lami zitaanza na safari za Kilimanjaro, Arusha, Zanzibar, Mwanza, Dodoma,
Tabora, Bukoba, Comoro, Dar es Salaam na Kigoma.
Madudu ATCL
Mbali na umuhimu wa unafuu wa ndege hizo, Rais Magufuli alitaja
madudu ya ATCL na mengine yanayofanywa nje ya Shirika hilo, huku akitamani
urais uwe wa miaka miwili ili ampe mtu mwingine, kwa kuwa kazi hiyo ni ngumu na
inamkosesha usingizi.
Rais Magufuli alitaja mambo yaliyomkera ATCL kuwa ni pamoja na
kutengenezwa kwa hasara kubwa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mafuta hewa,
kupoteza zaidi ya Sh milioni 700 bila wahusika kuchukuliwa hatua.
Alisema kampuni hiyo ilipata kukagua ndege iliyokuwa inakwenda
Tabora lakini ikagundua kuwa tairi ni bovu, lakini kutokana na ‘upigaji’
walilazimisha safari na ilipofika Tabora tairi lilipasuka wakaamua kukodi ndege
nyingine kwa dola 6,000 (Sh milioni 12) za Marekani.
Alisema viongozi na wakurugenzi walikuwa wanajilipa Sh 50,000 kwa
ajili ya kutembelea uwanja wa ndege, hivyo walikuwa wanatumia nafasi hiyo kurudia
kutembelea zaidi ya mara tatu na kujilipa posho za muda wa ziada.
Alisema ATCL ilikosa wafanyakazi wenye uamuzi na kujituma, huku
akivitaja vituo vilivyokithiri uozo huo kuwa ni Comoro, Mwanza, Mtwara na Dar
es Slaam.
Alisema kulikuwa na wafanyakazi pandikizi wa mashirika shindani,
tiketi za watoto zilitumika kwa watu wazima na kukatisha tiketi kupitia
mawakala, ili baadaye wawalipe asilimia ambazo waligawana.
“ATCL ilikithiri kwa kutofuata ratiba unaweza ukaambiwa ndege
inaondoka leo lakini ikaondoka jioni au kesho au hata wiki, hivyo abiria
walikata tamaa na kuona ubabaishaji ambao hauwasaidii.
“Kulikuwa na mafuta hewa, ndege ilikuwa inaonekana kuwa iko Mwanza kumbe
iko hapa hapa na imejazwa mafuta, wakubwa waliamua ‘kupiga dili’ walikuwa
wanasema ndege imejaa ili tiketi ziuzwe kwenye mashirika mengine … ambao hawafai
toeni nje,” aliagiza.
Alisema Sh milioni 700 zilipotea kituo cha Comoro, lakini hakuna
hatua zilizochukuliwa na mhusika aliyepoteza fedha ambaye alitakiwa kustaafu
Februari mwaka huu, aliongezwa muda ili aendelee kupoteza.
“Haiwezekani tununue ndege kwa gharama kubwa halafu watu watumie
kwa manufaa yao, ndege inakwenda na abiria watatu, wanne kumbe inakwenda
kufanya ununuzi wa mtu, nayajua yote,” alisema.
Utumbuaji
Alimtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa na Bodi ‘kutumbua’ bila kuwaonea huruma wafanyakazi wabovu.
Alisema aliondoa wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA) zaidi ya 500 hivyo hawezi kushindwa kuondoa wafanyakazi 200 huku kukiwa
na vijana wengi wanaotafuta ajira.
Wake wa viongozi
Rais Magufuli alisema wapo viongozi wakiwamo mawaziri ambao wake
zao wanafanya kazi katika Shirika hilo ambalo lilikuwa linaizalishia Serikali hasara.
“Wapo wake za viongozi, sisi wenyewe tumekuwa na tabia ya kuwekana,
wewe kama ni Waziri kwa nini mkeo aendelee kukaa katika Shirika ambalo halizalishi?”
Alihoji.
Ndege zingine
Alisema Serikali inajipanga kununua ndege zingine mbili ambazo moja
itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160 na nyingine abiria 240 na tayari fedha za
kununulia zipo.
0 comments:
Post a Comment