TETEMEKO la Ardhi lililotokea juzi katika mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara na kusababisha vifo na majeruhi, lina uhusiano na tukio la kupatwa kwa jua lililotokea Septemba Mosi mwaka huu, JAMBO LEO limeelezwa.
Hayo yalielezwa jana na wataalamu
wa miamba waliozungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili kuhusu tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augostino Olomi alisema kuwa hadi jana tukio
hilo limethibitika kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 170.
Kati yao majeruhi 83 wamepata matibabu
na kuruhusiwa kutoka hospitali.
Wataalamu hao kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam walieleza kuwa kupatwa kwa jua kunaongeza nguvu ya kuzalisha tetemeko
la ardhi, hasa kama tetemeko hilo lilikuwa linakaribia kutokea.
Ingawa watalaamu hao hawakueleza
kwa hakika tofauti ya muda inayohitajika ili tukio moja liathiri lingine,
tetemeko hilo la ardhi limetokea siku kumi tangu Jua lipatwe katika ardhi ya
Tanzania eneo la Rujewa wilayani Wanging’ombe katika mkoa wa Njombe.
Walichosema
Mhadhiri wa chuo hicho, Dk Richard
Wambura alisema kuwa ni dhahiri kwamba kupatwa kwa jua kuna uhusiano na
tetemeko la ardhi.
“Kupatwa kwa jua kunapunguza mvuto
wa dunia kwenye jua, kupunguza nguvu kunadisturb (sumbua) lakini haitoshi
kuzalisha tetemeko, ila inaweza kuchangia endapo lilikuwa (tetemeko) karibu
kuzalishwa na likawa halina nguvu,” alisema Dk Wambura.
Alisema kupatwa kwa jua kunaweza
kuongeza nguvu na kusababisha tetemeko la ardhi, kwani tukio hilo linachangia
msuguano wa miamba ambayo muda wote inakuwa inatembea.
“Tukio hilo sasa linatengeneza
sura ya Bonde la Ufa,” alisema. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, uwepo wa mwezi
katikati ya jua na dunia, husababisha umbo la dunia kubadilika kutokana na
kukosa mvutano wa moja kwa moja kwa sababu dunia huwa imekandamizwa na hivyo
kuzalisha vipande vilivyoungana.
“Vipande hivyo vikibonyezwa
husababisha msuguano ambao huzalisha tetemeko la ardhi.
Katika tukio la kupatwa kwa jua,
mwezi hukaa katikati ya dunia na jua, hivyo mvutano wa moja kwa moja wa dunia
na jua hupunguzwa na uwepo wa mwezi katikati ya sayari hizo,” alisema. Alisema
kupatwa kwa jua hakusababisha moja kwa moja kutokea tetemeko la ardhi,
isipokuwa linachangia kulifanya tetemeko lililotaka kutokea litokee kabla ya
muda wake.
“Mfano, kama tetemeko la ardhi
lilipaswa kutokea miaka mitano au miwili, kupatwa kwa jua kunaweza kusogeza
tukio hilo na kulifanya litokee kabla ya muda huo,” alisema Dk Wambura.
Aliaongeza ‘’Japokuwa uhusiano wa kupatwa kwa jua na tetemeko la ardhi una mchan-
go mdogo, moja likitokea linaweza kuathiri lingine,” alisema.
Alisema katika tetemeko la Kagera,
Kuna ufa unaopita kutokea Ziwa Victoria, Bonde la Magharibi Rwanda, Kigoma na
Nyasa ambao umezidiwa nguvu inayojikusanya kwa miaka mingi, ndiyo uliosababisha
tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa Ritcher 5.9 .
Historia ya matetemeko ya ardhi nchini
Dk Wambura alisema tetemeko lingine
kubwa la ardhi liliwahi kutokea eneo la Karema katika ukanda wa Ziwa Tanganyika
upande wa Bonde la Ufa. Tetemeko hilo lilitokea mwaka 1910 likiwa na ukubwa wa ritcher
7.4.
Alisema mwaka 2005 tetemeko lingine
lenye ukubwa wa ritcher 6.8 lilitokea Ziwa Tanganyika eneo la Karema na Karemee
ambayo ipo upande wa Kongo.
Alisema ukanda wenye Bonde la Ufa
mara kadhaa hurudiwa na tetemeko la ardhi kwani muda wote miamba inakuwa
inakusanya nguvu ambayo inasukuma hiyo miamba na kusababisha tetemeko la ardhi.
Dk Wambura alifafanua kuwa dunia
kama ilivyo sayari zingine, zilizo hai kuna miamba migumu juu yake na ndani ipo
miamba laini ambayo inaleta volcano.
Alisema matetemeko ya ardhi
yameendelea kutokea maeneo mengi ya nchi, lakini kwa kuwa hayakuleta madhara
makubwa hayakufahamika.
Alieleza kuwa mwaka 2009 lilitokea
tetemeko lingine katika maeneo ya Ziwa Natron. Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa
wa ritcher 5.9 na mwaka 2008 kulitokea tetemeko la ardhi mkoani Morogoro. Mwaka
huu limetokea tetemeko linguine mkoani Dodoma.
Naye David Kahumbi, alisema ikiwa
tetemeko la ardhi lilipaswa kutokea lakini likawa halina nguvu, kupatwa kwa jua
kunaweza kuchangia.
Alisema historia inaonyesha
tetemeko kubwa zaidi ya hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa ritcher 7.2 lilitokea
Julai 1919 katika Ziwa Tanganyika.
“Tetemeko lingine lilitokea Mwaka
2005 huko huko Kigoma katika Ziwa Tanganyika. Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa
wa Ritcher 6.8. Pia mwaka 2007 kulitokea tetemeko lingine katika mkoa wa Arusha
na Mashariki ya Bukoba nalo lilikuwa na ukubwa wa Ritcher 6.0’’ alisema.
0 comments:
Post a Comment