Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako |
“Kuna zaidi ya wanafunzi 16,000 ambao hawatapata fursa ya
kujiunga na chuo kikuu mwaka huu, kulingana na mwongozo wa sasa kwamba
waliopata alama mbili wasidahiliwe,” alisema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Baamoyo,
Profesa Costa Mahalu na kuongeza:
“Hiki ni kiama kwa vyuo vikuu binafsi, maana idadi ya
waliopata alama nne ni ndogo na inawezekana wote wakaenda kwenye vyuo vikuu vya
umma. Kibaya zaidi hakuna mahala ambako Serikali imepanga kuwapeleka hao ambao
hawatadahiliwa.”
Kauli ya Profesa Mahalu iliungwa mkono na wahadhiri
wengine kadhaa, waliosema kuwa kitendo cha Serikali kupandisha alama ya ufaulu
wa kujiunga na chuo kikuu, kitaongeza ‘vilaza’ badala ya kuwapunguza.
Mmoja wa wahadhili hao kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya
Tiba (IMTU), ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa si
msemaji wa chuo, alisema: “Mtu hawezi kuwa ‘kilaza’ akiwa chuo kikuu.”
Alisema: “’Ukilaza’ unaanzia elimu ya msingi na
sekondari. Jambo la maana hapa si kupandisha kiwango cha ufaulu ili kuondoa ‘vilaza’,
muhimu ni kuangalia mfumo wetu wa elimu kuanzia chini. Elimu yetu haisaidii
watoto kufanya kazi, inataka wawe na vyeti tu.”
Mhadhiri huyo alibainisha kuwa kwa sababu Serikali
haijaandaa mahala pa kupeleka wanafunzi waliopata alama mbili, sasa watatafuta
vyuo nje ya nchi kwa gharama ya vyuo vya ndani.
Alipoulizwa ilikuwaje ikakubalika wenye ufaulu wa alama
mbili wajiunge na vyuo vikuu na sasa imefutwa, mhadhiri huyo alijibu: “Ndiyo
maana nasema Waziri anakurupuka. Haya yalikuwa makubaliano kati ya vyuo na TCU.
Sasa yeye anakuja kuyatengua bila kupata ushauri.”
Kufunga vyuo
Katika hatua nyingine, baadhi ya wahadhiri wa vyuo vitano
vilivyofungwa kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2016/17 walimtuhumu Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako kwamba anatumika kuvihujumu.
Kwa nyakati tofauti wasomi hao walisema hakuna sheria inayompa Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, mamlaka ya kufunga vyuo, badala yake kupitia Tume ya Vyuo
Vikuu (TCU) anapaswa kuvieleza kasoro na kusimamia kuzisahihisha.
“Kuna mambo mengi ambayo sisi wadau tukiyaangalia
tunashindwa kuelewa waziri ana nia gani na elimu ya Tanzania. Amekuwa
akijiamulia mambo bila ushauri na kibaya zaidi anaingilia kazi za TCU,” alisema
mmoja wa wahadhiri hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alieleza
kuwa tangu Mei, Waziri amekuwa akifanya mambo matatu yanayoingilia utendaji wa
vyuo vikuu na hata kutia hofu kwamba chini ya uongozi wake, kiwango cha elimu
kitashuka.
Alitaja mambo hayo kuwa ni kuvifunga vyuo kudahili
wanafunzi mwaka huu wa masomo, sakata la wanafunzi hewa na kupandisha kiwango
cha ufaulu wa kujiunga na vyuo vikuu. Mapema Julai, Waziri Ndalichako
alitangaza kuvifunga vyuo vitano kudahili wanafunzi kwa madai kuwa havijakidhi
vigezo vya kuendesha kozi husika.
Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Bagamoyo (kozi
zote), Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba (IMTU), Chuo Kikuu cha Dodoma (Utabibu),
Chuo kikuu cha St. Francis na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar. Mmoja wa wahadhiri
wa vyuo hivyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa alichoeleza kuwa anaweza
kuandamwa na Waziri Ndalichako, alisema:
“Utadhani kuna uadui kati yetu na Waziri, kumbuka hakuna
sheria ya kufunga vyuo, lakini pamoja na kwamba tayari ameagiza tusidahili
wanafunzi mwaka huu, hatuna barua rasmi inayotuzuia kufanya hivyo.” Aliendelea
“Kuna hatua kadhaa ambazo lazima zipitiwe, moja, wanakuja wakaguzi ambao kibaya
zaidi wanaokagua vyuo hivyo wote wanatoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao ni
washindani wetu katika kutafuta wanafunzi.
“Kama watabaini kasoro wanakieleza chuo husika na
kukitaka kifanye marekebisho. Cha ajabu sisi tumefanya marekebisho na hawajaja
kukagua tena, lakini tunasikia tu kwamba tumefungwa.”
Mhadhiri huyo alipendekeza iwepo Bodi maalumu ya kukagua
vyuo, badala ya kutumia wakaguzi wa chuo kimoja cha Serikali ambao wanaweza
kuwa na maslahi binafsi.
“Mwaka huu UDSM ilianzisha kozi tatu mpya; Udaktari
Kilimo na Majenzi. Hapa unaona kwamba wanaleta ushindani katika vyuo vya
Sokoine, Ardhi na vingine vinavyoendesha kozi hizo. Kwa nini wasiwe na maslahi
wanapovikagua ili wawapoke wanafunzi?” Alihoji.
Wanafunzi hewa
Wahadhiri hao walisema uamuzi mwingine unaohatarisha uhai
wa vyuo vikuu binafsi ni kutafuta wanafunzi hewa kuanzia Mei.
“Utekelezaji wake umetuathiri sana kwa kuwa tangu Mei,
Bodi imesitisha mkopo kwa wanafunzi wote. Fikiria sisi (vyuo binafsi) tunajiendesha
kwa ada za wanafunzi, halafu Bodi inasitisha mkopo, tutalipaje mishahara ya
walimu, bili za umeme na maji?” Alihoji.
Aliendelea: “Julai 25, Waziri Ndalichako alikoleza moto
kwa kutoa agizo la kuzuia wanafunzi wa kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kwa
madai kuwa hakuna pesa. Wanafunzi wakaruhusiwa waende likizo, lakini baada ya
wiki mbili akatoa tena tangazo kuwa wanafunzi wanatakiwa kwenda kwenye mafunzo
hayo Agosti 8.
“Mwanafunzi aliye likizo utampata wapi asaini fomu ili
aingiziwe pesa za vitendo?. Maana pesa haiwezi kuingizwa mpaka asaini,” alihoji
na kubainisha kuwa maagizo kama hayo aliyoyaita ya kukurupuka, ndiyo yanayoleta
picha kwamba kuna wanafunzi hewa.
Mhadhiri huyo aliponda uamuzi wa Serikali kutumia
Takukuru kutafuta wanafunzi hewa vyuoni, akieleza kuwa hauna tija. “Kuna
wanafunzi wanatumiwa fedha halafu wanakuja kusaini baadaye, unamwitaje hewa
wakati tatizo hilo umelisababisha mwenyewe.”
Majibu ya Wizara
Waziri Ndalichako hakupatikana kuzungumzia suala hilo,
lakini Ofisa Habari wa Wizara, Oliva Kato alisema Waziri ndiye mwenye dhamana
na mambo yote yanayohusu elimu, hivyo uamuzi ule aliufanya kama mtu aliye na
mamlaka ya kusimamia elimu. “Kama Waziri ameingilia mamlaka ya TCU ambaye
angetakiwa kuleta malalamiko ni TCU, umeshasikia wamelalamika au unajua ukomo
wa majukumu ya Waziri?” Alihoji Kato.
Aidha, alisema kuhusu vyuo hivyo kutopelekewa barua rasmi
ya kusimamishwa kufanya udahili wa wanafunzi mwenye majibu ni TCU.
Kaimu Mkurugenzi wa TCU, Profesa Eliuter Mwageni
alipotafutwa kwa njia ya simu atoe majibu, alisema haamini kama anaongea na
mwandishi wa habari.
“Nitajuaje kama naongea na mwandishi, nitafute ofisini
tutazungumza,” alisema.
0 comments:
Post a Comment