* Dar pia si salama, hasa maeneo ya Mbagala
* Likitokea, mahali salama ni kona ya nyumba
WAKATI
Taifa likijikusanya kusaidia walioathirika kwa tetemeko la ardhi lililotokea
Jumamosi iliyopita mkoani Kagera, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), umetaja
mikoa kumi iliyo hatarini kukumbwa na janga hilo wakati wowote.
Mtendaji
Mkuu wa wakala huo, Profesa Abdulkarim Mruma alilimbia gazeti hili kuwa matetemeko
ya ardhi Tanzania ni jambo la kawaida kutokea kwa sababu nchi imepitiwa na
Bonde la Ufa lenye vitovu vya matetemeko.
“Tetemeko
si jambo la bahati mbaya kwa sababu kitaalamu hali hiyo inaweza kutokea wakati
wowote katika nchi zilizopitiwa na bonde hilo,” alisema Profesa Mruma.
Kuonesha
uhalisia wa uwezekano wa kutokea matetemeko zaidi nchini, Profesa Mruma alisema
tetemeko hilo la Kagera ni la pili kutokea mwaka huu, ambapo miezi miwili iliyopita
lilitokea lingine mkoani Dodoma lililokuwa na uzito wa skeli ya Richter 5.1.
Mikoa
ya Pwani
Katika Jiji
la Dar es Salaam, Profesa
Mruma alisema eneo la
Bonde la Mto Ruvu linaloanzia Mkoa wa Pwani hadi katika jiji hilo na katika bonde la Mto Mzinga, unaopita maeneo ya Mbagala, kuna kitovu cha tetemeko la ardhi, hivyo kuwa katika hatari ya kutokea wakati wowote.
Profesa
Mruma alisema Katika Ukanda huo wa Pwani, kitovu kingine cha tetemeko la ardhi
kiko katika fukwe za Bahari ya Hindi hasa katika Mkoa wa Mtwara, kwenye makutano
ya bahari hiyo na
nchi ya
Madagascar.
“Mkoa huu
(Dar es Salaam) pamoja na maeneo yote yaliyo katika Ukanda wa Bahari hayako
salama kwani pia yanaweza kutokewa na matetemeko ya ardhi,” alisema.
Mkuu wa
Idara ya Jiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Elisante
Mshiu, alipozungumza na gazeti hili wiki hii, naye alisema Jiji la Dar es Salam
haliko salama kwani linaweza kutokewa na matetemeko ya ardhi.
“Mkoa huu
pamoja na maeneo yote yaliyo katika Ukanda wa Bahari hayako salama, kwani pia
yanaweza kutokea na matetemeko ya ardhi,” alisema.
Kanda
ya Ziwa, Kati
Mbali na
Jiji la Dar es Salaam,
Profesa Mruma alitaja
Ukanda wa Ziwa Nyasa na hasa mikoa ya Ruvuma na Mbeya, ambako alisema kumepitiwa na Bonde la Ufa na kuna kitovu hicho, hivyo wakati wowote tetemeko linaweza kutokea.
Alisema
katika Ziwa Rukwa, Mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani inaweza kupatwa na tetemeko
hilo kupitia kitovu kilichoko katika ziwa hilo.
Mtaalamu
huyo alisema Mkoa wa Kigoma nao uko hatarini kutokana na kitovu kilichoko
katika Ziwa Tanganyika, huku Mkoa wa Kagera ukiwa hatarini kutokana na kitovu kilichoko
katika Ziwa Albert, nchini Uganda.
Profesa
Mruma aliutaja mkoa wa Dodoma kuwa nao upo hatarini kupata tetemeko la ardhi
katika kitovu kilichoko kwenye Mlima Chinene.
Mkoa
wa kumi
Profesa
Mruma alisema hadi Julai
2007 Mkoa wa Arusha
ulikuwa umepatwa na matetemeko 18 kutokana na kitovu kilichoko katika Milima ya Ol Doinyo Lengai, ambao wenyeji wake jamii ya Kimasai, wanautambua kuwa ‘Mlima wa Mungu’.
Pamoja na
kutaja mikoa hiyo kumi, Profesa Mruma alihadharisha kuwa tetemeko la ardhi
linalogusa Tanzania, linaweza pia kupata msukumo kutoka vitovu vilivyoko katika
nchi jirani, hivyo si lazima kitovu kiwe Tanzania.
“Kuna eneo
kama Ziwa Kivu katika nchi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ziwa
Albert, Uganda na Kenya na Ethiopia, yakiwa na tetemeko yanagusa hadi kwetu,”
alisema.
Dk Mshiu wa
UDSM katika hilo, naye alisema hata maeneo ya jirani na kitovu cha tetemeko,
yanaweza kuathirika.
Kwa mujibu
wa Dk Mshiu, athari katika maeneo au mikoa ya jirani, husababishwa na uelekeo
wa tetemeko kutoka katika kitovu, upande linakoelekea huathirika na eneo ambalo
halikuelekea, hakutaathirika.
Ukubwa,
upimaji
Akizungumzia
ukubwa wa matetemeko
ya ardhi yaliyokwishatokea nchini, Profesa Mruma alisema lililopiga Kagera si kubwa katika nchi, ingawa madhara yake ndiyo makubwa katika historia ya matetemeko nchini.
Tetemeko la
Kagera kwa mujibu wa Profesa Mruma, lilikuwa na ukubwa wa uzito wa skeli ya
Richter 5.7, wakati taarifa zinaonesha kuwa tetemeko kubwa lililowahi kutokea
nchini, lilifikia uzito wa skeli ya Richter 6.3 na lilipiga mkoani Mtwara.
Alipoulizwa
kwa nini tetemeko la Kagera limesababisha athari kubwa, wakati ni dogo ikilinganishwa
na la Mtwara, Profesa Mruma alisema madhara yaliyotokea Kagera, yamechangiwa na
nyumba nyingi kukosa ubora ikiwa ni pamoja na kutokuwa na linta.
Madhara
mengine alisema yanaweza kuwa yametokana na ukosefu wa teknolojia ya kutoa
taarifa za kutambua tetemeko wakati likitokea.
“Tetemeko
linatokea kwa sekunde hali inayochangia taarifa zake kutojulikana pale
linapotokea na hiyo ni moja ya sababu ya kuwep
madhara wakati mwingine.
“Teknolojia
iliyopo duniani kwa sasa ni ile inayotoa taarifa muda huo huo tukio likitokea,
pamoja na ukweli kuwa hakuna teknolojia inayoweza kutoa taarifa kabla ya tukio.
“Lakini
sisi bado tupo katika mfumo wa zamani wa kukusanya taarifa na baadaye ndio
tunazielezea kutokana na ukosefu wa mfumo wa mtandao kama walivyo wenzetu,”
alisema Profesa Mruma.
Profesa
Mruma alisema GST ina vituo tisa vyenye uwezo wa kukusanya taarifa baada ya
tukio, hivyo mikakati yao ni kuhakikisha wanakuwa na teknolojia ya kisasa ya sateliti,
iwasaidie kupata taarifa muda huo huo wakati tetemeko likitokea.
Kwa
nini tetemeko linatokea?
Akijibu
swali kuhusu kitu kinachotokea kitaalamu kabla ya tetemeko, alisema ni miamba
ya chini ya ardhi kuteleza kutokana na mgandamizo na kuhama umbali wa Kilometa
10 hadi 40.
Profesa
Mruma alisema tetemeko lililotokea Kagera lilitokea Kilometa 10 chini ya ardhi
na kusababisha madhara yaliyotokea, lakini kama lingetokea Kilometa 40 madhara yangekuwa
makubwa zaidi.
”Tetemeko
hilo lililotokea Septemba 10 mwaka huu majira ya saa 9:27, mchana kitovu chake
kilikuwa kati ya Latitudo 10 06’ na Longitudo 31055’ eneo ambalo ni Kilometa 20
Kaskazini Mashariki mwa Kijiji cha Nsunga na Kilometa 42 Kaskazini Magharibi
mwa Mji wa Bukoba,” alisema Profesa Mruma.
Kujikinga
Akielezea
namna ya kujikinga
tetemeko linapotokea,
Profesa Mruma alisema kwanza jamii inashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia viwango halisi vya ujenzi. Amewataka
wananchi kuweka
misingi imara wakati wa
ujenzi wa nyumba na kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo na kuepuka kujenga nyumba milimani.
Profesa
Mruma alisema tetemeko likitokea, mahali salama ambako mwananchi anashauriwa
kukaa ni sehemu ya wazi, isiyo na majengo marefu au miti mirefu au miinuko mikali
ya ardhi.
“Endapo
tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba, unashauriwa ukae chini ya uvungu wa meza
imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta.
“Ukiwa
ndani jiepushe kukaa karibu na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au
fenicha, ili usiangukiwe na vitu hivyo,” alisema Profesa Mruma.
Wananchi
pia wanashauriwa kuzima umeme katika majengo, ili kuepuka kutokea kwa hitilafu
ya umeme kama mitetemo itaendelea. Pia wametakiwa kukagua majengo kwa uangalifu
na kuhakikisha hawapati madhara baada ya tetemeko na kama yanaweza kuendelea kutumika,
ikibidi waite wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi.
0 comments:
Post a Comment