MWANASHERIA Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amejitosa kusaidia
watuhumiwa 83, wanaodaiwa kukamatwa kutoka maeneo mbalimbali nchini na
kushikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kwa kuisema vinaya
Serikali, ikiwa ni pamoja na kutumia neno dikteta.
Ametoa kauli hiyo jana alipozungumzana waandishi wa habari, katika
Makao Makuu ya chama hicho Dar es Salaam, kuhusu mambo yanayoendelea kutokea
tena kimnya kimnya nchini.
Alidai kuwa watu hao wamekamatwa kutoka maeneo mbalimbali nchini
kwa agizo la wakuu wa Polisi, huku wengine wakiteswa kwa madai kuwa wameandika
kauli zinazomhusu Rais John Magufuli na utendaji wake katika mitandao ya
kijamii.
Alitaja waliotoa maagizo hayo kuwa ni Inspekta Jenerali wa Polisi
(IGP) Ernest Mangu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Diwani
Athumani, Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro na makamanda
kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa madai ya Lissu, kukamatwa kwa watu na kuteswa
kutokana na sababu zinazohusu Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta)
na hali ya kisiasa nchini tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani,
kunazidi kushika kasi.
Alidai kati ya watu hao, watuhumiwa kumi amewatembelea walipo; nane
wapo Kituo cha Polisi Olysterbay na wawili Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es
Salaam huku watu wengine 73 taarifa zikikosekana kuhusu vituo walikopelekwa.
Lissu aliwataja kwa majina watu hao nane ambao wapo Kituo cha
Polisi Oysterbay kuwa ni Aristotle Ngasi, Hosia Mbuba , Ignasia Mzenga, Shakira
Abdallah Makame na Dk David Nicas ambaye alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Busega
2015.
Wengine ni Mdude Nyangali, Juma Salum na Suleiman Said na wawili
wanaodaiwa kuwa Kituo Kikuu cha Polisi ni Ben Nzogu na Mussa Sikabwe.
Kwa mujibu wa madai ya Lissu, waliopo wa Kituo cha Oysterbay
wamemweleza kuwa wamekuwa wakipata manyanyaso ya hali ya juu wakiwa mahabusu.
Alidai watu hao walimweleza kuwa wamekuwa wakitolewa mahabusu usiku
na kupelekwa katika eneo la Mikocheni, ambako kuna kikosi kazi kinachojumuisha
Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, ambao kazi yao ni kuwapiga na kuwatesa.
“Nchi si kwamba haina sheria zinazokataza mambo hayo na si kwamba
yanayofanywa na Polisi hayakatazwi. Katiba ya Nchi ibara ya 13 kifungu kidogo
cha 6 I, kinaeleza kuwa ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au
kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha,”alisema.
Alisema kupitia ibara hiyo ni wazi kuwa jeshi hilo linakiuka Katiba
kutokana na kuwa kutoa habari kunalindwa na Katiba si Serikali ya Rais
Magufuli. Aliongeza kuwa jambo la kushangaza, kuna baadhi ya watu hao wamekaa
mahabusu kwa siku 46 bila kupelekwa mahakamani, jambo ambalo ni kinyume cha
sheria na ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwani kisheria inabidi mtu akae
mahabusu saa 24 tu.
“Kama watu hao wangekuwa kizuizini kwa kauli ya Rais, tungesema
kuwa ni kizuizi kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1962 lakini kwa kuwa ni kwa
mujibu wa Jeshi la Polisi ni ukiukwaji wa Katiba,” alisema.
Alisema kama watu hao hawataachiwa huru Jumanne ijayo, hasa wale 10
ambao wanafahamika au kama watakuwa hawajapelekwa mahakamani au kuachiliwa kwa
dhamana ya Polisi, chama hicho kitakwenda Mahakama Kuu kufungua maombi kwa mujibu
wa utaratibu wa sheria.
Alifafanua kuwa kifungu cha 390 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai, kinaruhusu Mahakama Kuu kutoa amri ya kuelekeza mtu ambaye anashikiliwa
kinyume cha sheria, kuletwa mahakamani au kuachiwa huru.
“Tunataka viongozi hao waseme ni lini Katiba imeruhusu wafanye
hivyo, maana kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti kifungu cha 32 inaeleza kuwa
halitakuwa kosa kutoa kauli ambazo lengo lake ni kuonesha Serikali imekosea na
hatujafanya kosa la jinai, hivyo waliokamatwa kwa kosa hilo hawana
kosa,”alisema na kuongeza.
“Kwa maoni yangu ni kuwa hakuna kosa pale, hivyo nitaisema kauli
yangu popote na muda wowote labda nisiwe hai na hakuna mahabusu itakayonifunga mdomo.”
Gazeti hili lilimpigia simu IGP Mangu, ilia toe ufafanuzi wa madai
hao, lakini ilipokewa na msaidizi wake aliyeagiza atafutwe msemaji wa Jeshi la
Polisi, Advera Bulimba, ambaye alielekeza makamanda wa mikoa ya kipolisi, Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam ndio wazungumze. Hata hivyo makamanda hao simu zao
ziliita bila majibu.
0 comments:
Post a Comment