IGP Ernest Mangu |
Usiku wa Agosti 26 polisi waliokuwa wakifuatilia
majambazi waliovunja na kuiba katika benki ya CRDB Mbande, Dar es Salaam,
walijikuta katika mapambano na majambazi hao waliowakuta eneo la Vikindu
wilayani Mkuranga.
Uchunguzi wa JAMBOLEO umebaini kuwa baadhi ya
wafanyabiashara sasa wanafunga maduka yao mapema, huku wakazi wake wakilazimika
kurudi majumbani mapema zaidi ikilinganishwa na kabla ya tukio hilo.
Wakati staili ya maisha ikionekana kubadilika, nyumba
iliyoshambuliwa na polisi, imeonekana kutelekezwa, baada ya vifaa vyake
kuendelea kuwa nje ya nyumba hiyo tangu siku hiyo, huku taa zake zikiwa
zinawaka muda wote.
Maduka kufungwa
Mwenyekiti wa Kijiji cha Vikindu Mashariki, Mohammed
Maundu alisema hali katika kijiji hicho ni tofauti ikilinganishwa na awali
kutokana na baadhi ya maduka kufungwa mapema. Alisema mbali na maduka kufungwa
mapema, ya karibu na nyumba kulikofanyika mapambano hayo, bado yameendelea kufungwa
kutokana na wamiliki kuchukuliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya maduka yakiwa na
makufuli, huku baadhi ya wahusika wakishikiliwa na Jeshi hilo.
Mwenyekiti huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara
wanafanya biashara zao kwa uoga na waendesha pikipiki wamekuwa wakisitisha
huduma hiyo giza linapoingia kutokana na uoga.
Hatukuwajua watu hao
Mwenyekiti huyo alisema hakuwafahamu watu wanaodhani kuwa
ni majambazi, ingawa taarifa alizopata baadaye zilieleza kuwa walikuwa hapo
siku nyingi.
“Kuna watu wanasema watu hao walikuwa hapo karibu miaka
mitatu sasa na wengine wanasema wana miezi sita tu. Mimi sina hakika kwani sikuwafahamu
kabla,” alisema Mwenyekiti huyo ambaye alimtupia lawama mjumbe wa eneo hilo kwa
alichosema ni kutompa taarifa mapema.
Mgogoro wa viongozi
Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa hana ushirikiano mzuri
na viongozi wenzake wa Serikali na hili lilitokana na mseto unaounda Serikali
hiyo ya kijiji. Alisema katika kipindi cha mfumo wa chama kimoja viongozi
walielewana, lakini sasa mfumo wa vyama vingi katika eneo hilo umesababisha
changamoto.
Alipata taarifa za ujambazi? Mwenyekiti huyo alieleza
kuwa alipigiwa simu na kuitwa eneo la tukio ambako alifika saa tatu asu-buhi.
“Kiutaratibu suala hilo ndivyo linavyofanyika lakini jambo lililonishangaza ni
baadhi ya wananchi kuwa na fikra tofauti na kuhisi kwamba Mwenyekiti huyo
anahusika kwenye suala hilo,” alisema.
Mwenyekiti alitoa mwito kwa viongozi wa eneo hilo,
hususan wajumbe wa nyumba 10 kushirikiana katika masuala mbalimbali,
akibainisha kuwa jukumu la kulinda amani ya eneo linaanzia kwao.
“Hatuwezi kulinda wenye silaha za moto, lakini vibaka
inawezekana na ni jambo la kitaifa, hivyo inabidi viongozi wa eneo hili na
kwingine kushirikiana nasi badala ya kumwachia majukumu mtu mmoja,” alisema.
Gazeti hili lilishuhudia vitu vikiwa vimetawanywa na
kutelekezwa nje ya nyumba hiyo. Ndani ya vyumba kulikuwa na vitu kama
vyerehani, nguo za watoto, mabegi, majiko, matundu ya vyoo yalikuwa wazi, paa
la nyumba liliharibiwa lote huku ukimya ukitawala katika aneo hilo.
0 comments:
Post a Comment